Waziri wa Kilimo afuta Siku ya Maadhimisho ya Wakulima Nanenane kwa mwaka 2021

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf F. Mkenda (Mb) ametangaza kufutwa kwa Sherehe za Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kwa Mwaka 2021 zilizokuwa zifanyike mwezi Agosti, 2021 katika kanda nane katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara, anaripoti Mwandishi Diramakini (Dodoma).

Prof. Mkenda ametoa tamko hilo leo Februari 10, 202 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba Serikali inakusudia fedha zote za umma zilizokuwa zimetengwa na wizara za kisekta na taasisi zake kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za Nane nane 2021 zitumike kuimarisha huduma za ugani nchini.

“Shughuli zote za Nanenane mwaka huu 2021 zimefutwa rasmi na Serikali na hivyo fedha zote zilizotengwa kwa kazi hiyo zitatumika kuboresha huduma za ugani nchini ili kuleta mapinduzi ya kilimo. Shughuli za Nanenane lazima ziendane na upatikanaji wa huduma bora za ugani hivyo lazima tujipange vema,"amesema Prof. Mkenda.

Waziri huyo wa Kilimo ameongeza kwa kusema, kufuatia uamuzi huo wa Serikali, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau itatumia muda huu kufanya tathmini ya namna maonesho ya Nanenane yamekuwa yakifanyika na kuona maeneo ya kuboresha ili yawe na tija katika kukuza sekta ya kilimo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla. Aidha, Prof. Mkenda alieleza kwamba Wizara ya Kilimo itaunda Kikosi Kazi Maalum kwa ajili ya kufanya tathmini hiyo ili kilete mapendekezo yatakayokuwa na tija katika maadhimisho ya Nane nane katika miaka ijayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mkenda amesema Wizara yake inaendelea kupitia zao moja hadi lingine yakiwemo ya kimkakati ili kuweza kutatua changamoto zilizopo na kuongeza tija na kipato kwa mkulima na Taifa kwa ujumla. Prof Mkenda aliongeza kuwa, tayari Wizara imefanya mapitio ya mazao kama ngano, alizeti, michikichi, tumbaku, kahawa na miwa kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji ikiwa ni pamoja na kupata masoko ya uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news