Taasisi ya Wezesha Foundation inayojihusisha na masuala ya uwezeshaji vijana na Wanawake imefungua kituo maalumu cha kuongeza ujuzi (Skills hub ) mkoani Kigoma, anaripoti Mwandishi Diramakini (Kigoma).
Kituo hicho kitajihusisha na utoaji wa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake katika uongozi na shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo hicho, Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Mhe. Zainab Katimba (Mb) amesema, mbali na kutoa mafunzo hayo kituo hicho kitakuwa kikitoa taarifa za fursa mbalimbali za Vijana na Wanawake katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni pamoja na kusaidia walengwa kunufaika na fursa hizo.
Aidha taasisi hiyo imetoa mashine 14 za kukoboa na kusaga nafaka kwa vikundi saba vya mfano katika halmashauri saba mkoani Kigoma. Lengo kuu likiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuwawezesha vijana na Wanawake kiuchumi.
Taasisi hiyo ambayo imeanzishwa mwaka 2017 tayari imefanya shughuli mbalimbali mkoani humo ikiwemo kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake zaidi ya elfu moja, mafunzo ya uongozi kwa madiwani wanawake, kutoa misaada katika sekta ya elimu na afya.
Tags
Habari