WIZARA YA ARDHI YAJA NA MKAKATI KUPIMA ARDHI NCHI NZIMA

Katika kuhakikisha ardhi ya Tanzania inapangwa na kupimwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuja na mkakati wa kuwatumia wapima wa kati (Para Surveyors) na vyuo vyake vya ardhi vya Morogoro na Tabora katika kuharakisha upimaji wa ardhi nchini,anaripoti Munir Shemweta (WANMM).
Akijibu hoja za Wabunge tarehe 13 Januari 2021 katika kikao cha Bunge, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema, mpaka sasa asilimia 25 tu ya ardhi ya Tanzania imepimwa ikijumuisha viwanja 2,349,626 na mashamba 28,312 huku jumla ya hati 1,559,609 zikiwa zimetolewa.

Amesema, kutokana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa na watumishi wachache 1400 kati ya 2500 wanaohitajika aliowaeleza kuwa hawezi kukidhi haja katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kusisitiza kuwa wameona waanze kutumia wapima wa kati pamoja na vyuo vya ardhi kutekeleza azma ya kupima ardhi nchini.

Amesema, Wizara yake ilijaribu kutumia Makampuni ya Upimaji katika zoezi la upimaji shirikishi lakini kati ya makampuni 134 yaliyopewa kazi ni makampuni 34 tu ndiyo yaliyofanya vizuri wakati wa utekelezaji zoezi hilo.

"Wizara sasa itaelekeza nguvu katika ofisi za mikoa kwa kuwa zina wataalam wote zishirikishe halmashauri zote ili kazi ya upimaji ifanyike kwa operesheni maalum kwa kuunda timu ndani ya mikoa na kuanza kushambulia wilaya moja hadi nyingine" alisema Dkt Mabula.

Akigeukia suala la ukusanyaji madeni ya kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa sugu, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, Wizara yake sasa itaanza kusimamia sheria kama kuwafikisha wadaiwa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya sambamba na kuwanyang'anya milki wale wote watakaokaidi kulipa madeni miezi sita baada ya kupelekewa ilani za madai.

Kwa mujibu wa kifungu Na 48(1) (g) cha sheria ya ardhi, Afisa Ardhi anayo mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi kwa mmiliki aliyekaidi kulipa kodi ya pango la ardhi katika kipindi cha miezi sita baada ya kutumiwa ilani ya madai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news