Timu ya Coastal Union imeiondoa Yanga SC katika mstari baada ya kuwachapa 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ndani ya Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, anaripoti MWANDISHI (Mkwakwani).
Yanga SC huu unakuwa mchezo wa Kwanza kupoteza msimu huu na kwa ushindi huo, Coastal Union inafikisha alama 26 baada ya kucheza mechi 22 na kupanda kwa nafasi tano hadi ya 10.
Aidha, pamoja na kufungwa, Yanga SC inabaki na alama zake 49 baada ya kucheza mechi 22 sasa huku ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa alama nne zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC.
Mchezo huo umechezeshwa na refa Raphael Ikambi aliyesaidiwa na Abdallah Rashid na Makame Mdogo ambapo Coastal Union walipata bao lao la kwanza kupitia kwa kijana alyeubuliwa timu ya vijana ya Yanga, Erick Msagati dakika ya 10.
Msagati alifunga bao hilo dakika moja tu baada ya kiungo Tuisila Kisinda, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuikosesha Yanga bao la mapema baada ya kumpelekea mikononi mkwaju wa penalti kipa wa Coastal Union, Abubakar Abbas Ibrahim kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa kwenye boksi.
Lakini Kisinda, mchezaji huyo wa zamani wa AS Vita ya kwao, Kinshasa akasawazisha makosa yake baada ya kuifunga Yanga SC bao la kusawazisha dakikia ya 39 kwa juhudi binafsi kufuatia kuwazidi maarifa mabeki wa Coastal.
Chipukizi Mudathir Said akawainua juu Coastal Union kwa bao la ushindi dakika ya 84 akitumia udhaifu wa safu ya ulinzi ya Yanga.
Aidha, mechi nyingine za Ligi Kuu ni pamoja na Polisi Tanzania imeichapa KMC 1-0 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Huku Tanzania Prisons ikilazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City Uwanja wa Samora, Sumbawanga mkoani Rukwa na Mtibwa Sugar wametoa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro
Kabla ya hapo, Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa Kataba Bukoba.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na kiungo Bryson Raphael dakika ya 20 na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube dakika ya 27, wakati la Kagera Sugar limefungwa na Peter Mwalyanzi kwa penalti dakika ya 42.
Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 22, ingawa inabaki nafasi ya tatu sasa ikizidiwa pointi tano na mabingwa watetezi, Simba SC walio nafasi ya pili japo wana mechi tatu mkononi.
Dodoma Jiji FC imeibuka na ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani mabao ya Dickson Ambundo dakika ya 35 na Peter Mapunda dakika ya 70.
Wakati huo huo, katika uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga, bao pekee la Nzigamasabo Steve dakika ya 61 limeipa Namungo FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC.
Huku uwanja wa Highland Estate huko Ubaruku, Mbarali mkoani Mbeya, Gwambina FC wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Ihefu SC.
Mabao ya Gwambina yamefungwa na Rajab Athumani dakika ya 19 na Paul Nonga dakika ya 74, wakati la Ihefu SC limefungwa na Andrew Simchimba dakika ya 90.
Tags
Michezo