Hayati Magufuli aacha simanzi, vilio nchini Malawi

Katika hali inayoonyesha Dunia imeguswa na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli wananchi nchini Malawi wamejawa na simanzi huku wakionesha kusononeshwa na tukio hilo la ghafla, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Chitipa).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa uhai wake akishuka ndani ya ndege mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa ndege wa Kimataifa wa Kamuzu uliopo Lilongwe nchini Malawi katika ziara yake mwezi Aprili 24, 2019. (Picha na Ikulu).

Hayati Dkt. Magufuli alifariki Machi 17, 2021 wakati akiwa katika matibabu ya matatizo ya moyo katika Hospitali ya Mzena iliyopo mkoani Dar es Salaam.

Kwa nyakati tofauti katika mji wa Chitipa wananchi hao wameieleza DIRAMAKINI kuwa, Hayati Dkt.Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyekuwa na mtazamo wa kujenga uhusiano wa kweli, imara na wa kudumu kati ya nchi hizi mbili.

Miongoni mwao ni Meshaki Limbewe ambaye amesema, walimfahamu Hayati Magufuli kwa kuwa alikuwa ni mtu wa kazi na mwenye kupenda sana watu wake hasa pale alipoamua kushughulika kero na matatizo ya watu wa chini kabisa.

"Hata sisi majirani zake wa Malawi alitupenda sana ndio maana aliamua kujenga barabara ya lami kutoka MpembaTanzania hadi mpakani pale boda Isongole ambayo imetusaidia sana sisi kufikia soko zuri la mahindi,"amesema Limbewe.

Amesema, uamuzi wa Hayati Magufuli kujenga barabara hiyo ulilenga kuimarisha uhusiano wa wa kweli kati ya mataifa haya mawili.

Kwa upande wake mkazi wa Chitipa, James Phili amesema, licha ya kwamba hakuwahi kufanikiwa kukutana ana kwa ana na hayati Dkt. Magufuli lakini alimfahamu kama kiongozi imara na mwenye msimamo usioyumba.

"Binafsi ninasononeka sana, lakini kwa kuwa kifo ni jambo lisiloepukika tunatakiwa sisi na majirani zetu wa Tanzania tukubaliane nalo, kwani kuna wakati unatamani kama kungekuwa na sehemu wanauza spea za moyo tungenunua turudishe uhai wake,"ameeleza kwa hisia kali Phili.

Phili ametumia nafasi hiyo kuonesha wasiwasi wake juu ya umaliziaji wa kazi ya ujenzi wa daraja la Isongole linalounganisha nchi hizo katika mto Songwe.

"Mwaka huu alitufanya tuwe na soko zuri la mahindi baada ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mpemba hadi Isongole kukamilika, sasa sijui itakuwaje sehemu ile ya daraja,"amesema.

Amewaomba vingozi wa serikali ya Tanzania kuona umuhimu na kumalizia sehemu hiyo ya ujenzi wa Daraja ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa ustawi wa maendeleo na biashara kati Malawi na Tanzania.

Serikali ya Tanzania imetumia kiasi cha shilingi Bilioni 107.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mpemba hadi Isongole kuunganisha nchi jirani ya Malawi , ikiwemo mita 300 ndani ya nchi ya Malawi ambayo ni kiungo muhimu kwa biashara baina ya pande hizo mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news