Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi mahiri na ameacha alama Taifa zima na ndiyo sababu analiliwa na wananchi nchi nzima hadi vijijini, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mwanza).
Ameyasema hayo leo Machi 24, 2021 alipozungumza na wananchi kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya shughuli za kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli ambayo iliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
”...Mpendwa wetu kaka yetu kiongozi wetu Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi shupavu aliyeliongoza Taifa hili kwa umahiri mkubwa na Mwanza ni mahali pa kihistoria kwa kiongozi wetu, ameishi hapa, amefanya kazi hapa na katika utumishi wake amefanya mambo makubwa ambayo yameweka alama kwenye mikoa hii ya Kanda ya Ziwa,"amesema.
Akiwasilisha salamu za Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema Rais anawapa pole Wanakanda ya Ziwa na anawasihi katika kipindi hiki cha majonzi wawe watulivu, waendelee kushikamana, kushirikiana na kupendana kama ilivyokuwa awali.
Amesema kila mwananchi kwa dini yake na dhehebu lake aendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Hayati Dkt. Magufuli pahala pema.
Waziri Mkuu amesema baada ya viongozi kumaliza kuaga, mwili utazungushwa katika uwanja huo ili kutoa nafasi kwa wananchi kumuaga Hayati Dkt. Magufuli na kisha mwili utazungushwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya mwili huo kuzungushwa katika jiji hilo, utaelekea Chato mkoani Geita kwa kupita katika daraja la Kigongo-Busisi na mwili utakapofika hapo utasimama kwa dakika kumi ili kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo ambapo ni nyumbani kwa mke wa marehemu kuaga mwili wa hayati Dkt. Magufuli.
Mapema asubuhi, Mheshimiwa Majaliwa aliwaongoza viongozi mbalimbali na wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kuupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Vilio, huzuni na simanzi zilitawala kwa wananchi waliojipanga pembezoni mwa barabara kuanzia uwanja wa ndege wa Mwanza hadi uwanja wa CCM Kirumba, ambapo ulipofika katika eneo la Nyamanoro ambako marehemu aliwahi kuishi msafara ulisimama ili kutoa fursa kwa waliokuwa majirani kumuaga.
Hayati Dkt. Magufuli alifariki dunia Jumatano Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Ijumaa Machi 26 wilayani Chato mkoani Geita.
Tags
Habari