Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ili kuyafikia maendeleo na uchumi unaohitajika, ni lazima kuhakikisha kuwa mazingira ya nchi yako sawa, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).
Akizungumza na Watendaji wa Idara ya Mazingira Machi 17,mwaka huu Mheshimiwa Othman amewaambia wanapaswa Zanzibar kujikita katika kuweka mazingira ya nchi kuwa salama kwani “uchumi na maendeleo yatakuja kama mazingira yatakuwa rafiki.“
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alikuwa ametembelea Idara hiyo, ambayo ni moja ya taasisi zilizo chini ya ofisi yake na yenye makao yake kwenye eneo la Maruhubi kando kidogo ya kitovu cha Mji wa Unguja, kwa lengo la kutambuana na kuangalia utendaji kazi.
"Nimesikiliza kwa makini majukumu yenu na mambo makubwa muliyoyafanya, ila niendelee kuwasisitiza kwamba mazingira yakiwa salama, basi uchumi wa nchi utapanda tu," amesema Mheshimiwa Othman ambaye kwenye ziara hiyo aliambatana na Waziri wa Nchi katika Ofisi yake, Mheshimiwa Saada Mkuya.
Akimtambulisha wafanyakazi na vitengo vya Idara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Bwana Sheha Mjaja Juma, alisema mpaka sasa wao wamefanikiwa kusimamia mazingira katika zoezi la utafutaji mafuta na gesi asilia.
“Tumefanikiwa pia kwa kiasi kikubwa kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki, sambamba na kutoa elimu ya mazingira kwa kuanzisha klabu za mazingira katika jamii na hata katika maskuli,"amesema Mkurugenzi huyo.
Miongoni mwa masuala tete yaliyojitokeza kwenye ziara hii, ni lile la maeneo ya pwani yanayoliwa na bahari na pia ardhi iliyokuwa ikitumiwa na Wananchi na kisha kutelekezwa.
Kuhusiana na maji ya bahari kula ardhi kunakotokana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, Makamu huyo wa kwanza wa Rais alitaka hatua za haraka zichukuliwe.
“Yapo maeneo ya wazi ambayo yalitumiwa na Wananchi na baadaye wakayatelekeza kwa kuamini ni mali ya serikali, hivyo hawawezi kuyauza na wengi wao hawayaendelezi. Hivyo ipo haja ya kuzungumza na Wizara ya Kilimo ili kuweza kuyatumia katika kilimo na kukuza uchumi wa Nchi,“ alielekeza.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais aliwahakikishia watendaji hao wa Idara ya Mazingira kwamba atalishughulikia suala la ofisi hiyo ili liweze kupatikana jengo la kisasa na lenye kutosheleza kwa matumizi ya Idara.
"Eneo la kazi likiwa zuri, basi hata ufanisi wa kazi na heshima huongezeka. Hivyo ipo haja ya haraka kulishughulikia suala la upatikanaji wa jengo zuri," amesema Mheshimiwa Othman, ambapo pia amewataka watendaji hao kujenga umoja na mshikamano katika utendaji wao kazi ili kuleta ufanisi wa Idara na serikali kwa ujumla.