Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman ametoa kauli hio leo Machi 4, 2021 alipokuwa akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu waliojitokeza katika Hitma (Dua) ya kumuombea Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia mwezi uliopita, anaripoti MWANDISHI (Mkoa wa Mjini Magharibi).
Dua hiyo iliyoandaliwa na Uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mjini Kichama ilifanyika katika Mskiti wa Muembe Tanga Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo pia ilihudhuriwa na viongozi wa wakuu wa Chama cha ACT Wazalendo pamoja na viongozi wa Kiserikali.
Akimkaribisha Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Chama cha ACT Wazalendo Makamu MwenyeKiti wa Chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Mhe Juma Duni Haji amesema Maalim alikuwa anawapenda sana Wazanzibari na alikuwa na lengo kubwa la kuwaunganisha, sasa kwa vile ameshatangulia na kwa sababu ameshapatikana kiongozi mwingine Mhe. Othman basi wampe ushirikiano na wawe pamoja nae, na hii ndio njia ya kumuenzi Maalim Seif.
Mhe.Othman amesema sio jambo rahisi kuvaa viatu vya Marehemu Maalim Seif ila kwa sababu Wazanzibari ni wamoja na wanaamini katika ushirikiano itakuwa rahisi kwake kufanikisha majukumu yake.
Mhe. Othman amesema Maalim Seif alikuwa ni muumini wa umoja na mshikamano hivyo wananchi kwa pamoja wakisimamia misingi hio watakuwa wamemtendea haki, na kwake ni faraja.
”Jambo muhimu kuliko yote ni kusimamia Umoja na Mshikamano baina yetu, kwani hilo ndio jambo kubwa ambalo Kiongozi wetu Maalim Seif alikuwa analihubiri, hivyo njia adhwimu ya kumuenzi ni kukiendeleza alichokiacha,”amesema Mhe.Othman.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesisitiza tena kwa kusema kwa hakika ni ngumu kuwa kama Maalim Seif, kwani Maalim ni Kitabu kilichokamilika na amefanya mengi sana enzi za uhai wake, lakini jambo kubwa linalompa moyo na faraja ni kwamba wapo viongozi wenzake ambao anaamini watashikamana na kushirikiana ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, kwani Wazanzibari kwa sasa wanapigania mustakbali wa nchi yao, na katika hilo Mungu hutia baraka na nguvu.
“kwasasa Wazanzibari tumepata fursa ya kuwa na Rais ambae amejipambanua katika kuikwamua Zanzibar kutoka hapa ilipo sasa, hivyo ipo haja mahususi Wananchi wote kwa pamoja kutazama mbele na kuisaidia Nchi yetu ili tuweze kukwamuka kwa kumuunga mkono Mh.Rais na Serikali kwa ujumla,"amesema.
Mhe. Othman alitoa shukrani tena kwa waandaaji wa shughuli hiyo na kuwataka Wananchi kila wanapopata fursa basi kuendelea kumuombea dua Maalim Seif Sharif Hamad.