MBUNGE KANYASU AMLILIA WAZIRI NDALICHAKO ULIPWAJI BILIONI1.7/- WAFANYABIASHARA GEITA

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu ameiomba Serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kumrejeshea Mkataba wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) cha mjini Geita Kampuni ya Skywards Company Limited ili aweze kupata uwezo wa kulipa wananchi 40 wanaomdai zaidi ya shilingi Bilioni 1.7,anaripoti Robert Kalokola (DIRAMAKINI) Geita.

Wananchi wapatao 40 wanadai Kampuni ya Skywards zaidi ya Bilioni 1.7 kutokana na kuikopesha bidhaa mbalimbali na huduma wakati ikitekeleza ujenzi wa chuo cha ufundi katika mtaa wa Mine mpya mjini Geita na kuondoka bila kuwalipa na kuvunjika mkataba baina ya kampuni hiyo na Mamlaka ya vyuo vya ufundi nchini (VETA).
Constantine Kanyasu Mbunge wa Jimbo la Geita mjini akisikiliza wafanyabiashara waliofika ofisini kwake wanaodai Bilioni 1.7 kwa Kampuni ya Skywards.(Picha na Robert Kalokola/ DIRAMAKINI).

Mbunge Constantine Kanyasu ametoa ombi hilo kwa Waziri Joyce Ndalichako baada ya kukutana na wafanyabiashara waliotoa huduma mbalimbali kwa kampuni hiyo na wamefikisha malalamiko yao ofisini kwake.

Akizungumza na wafanyabiashara hao Kanyasu amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakidai kiasi hicho cha fedha kwa muda mrefu sasa na bila mafanikio ya kulipwa fedha zao.

Kanyasu ameongeza kuwa uchunguzi wa VETA kuhusu suala hilo dhidi ya mkandara limechukua muda mrefu bila kutoa matokeo ambayo yangesaidia wafanyabiashara hao kupata haki zao.
Baadhi ya wafanyabiashara wakimsikiliza mbunge wa Jimbo la Geita mjini Constantine Kanyasu (hayuko pichani) walipofika ofisini kwake kumueleza madai yao ya bilioni 1.7 kwa kampuni ya Skywards (Picha na Robert Kalokola/DIRAMAKINI).

Aidha Kanyasu amefafanua kuwa, kampuni hiyo inaonekana haina tatizo lolote la kiufundi au kujenga kwa kiwango cha chini,bali inadaiwa kuwa ilikuwa na mapungufu kwenye kuwasilisha taarifa za vifaa (mitambo) na wataalam wa kampuni.

Hata hivyo ameeleza kuwa mambo kama hayo yasingezuia Mkandarasi kuendelea na ujenzi huo ,na kuomba waziri wa Elimu kuingilia kati ili ujenzi huo uendelee na wananchi hao walipwe.

Kiongozi wa wafanyabiashara hao wanaodai, Godfrey Barinako amesema kuwa jumla ya madai yao ni Bilioni 1.7 na wako wananchi 40 ambao walikuwa wanatoa huduma mbalimbali kwenye kampuni hiyo wakati inajenga chuo hicho.
Godfrey Balinako Kiongozi wa wafanyabiashara 40 wanaodai Kampuni ya Skywards zaidi ya Bilioni 1.7.(Picha na Robert Kalokola/DIRAMAKINI).

Amesema baadhi yao ni wafanyabiashara ambao walitoa huduma ya bidhaa kama saruji,nondo, tofali na mabati.

Wengine ni mama lishe waliokuwa wanatoa huduma ya chakula,vibarua wa ujenzi,kukodi magari ya kusomba mchanga, kokoto,mawe na walinzi .

Amesema wameona wakimbilie kwa mbunge wao ili aweze kifikisha kilio chao kwa waziri husika ili serikali iweze kuwasaidia kupatikana kwa fedha yao.

Amesema kuwa kwasasa wanakabiliwa na matatizo ya kudaiwa na taasisi za kifedha Kama benki na mamlaka ya mapato (TRA) kwasababu mitaji yao imeshikiliwa huko bila kulipwa.

Amedai kuwa baadhi ya watu wanaodai Kampuni hiyo ni wagonjwa,wengine Wana hali mbaya kimaisha kwasababu mtaji wote uliisha huku baadhi yao wakishindwa kupeleka watoto shule.

Naye mfanyabiashara wa mbao Mussa Makumiane amesema alitoa bidhaa ya mbao yenye thamani ya milioni 17.8 kwa kampuni hiyo lakini baada ya kuvunja mkataba na veta iliondoka bila kumlipa chochote hadi sasa.

Makumiane ameiomba serikali kumrudishia mkataba wa ujenzi mkandarasi huyo ili aweze kuwalipa fedha hizo na wao waendelee kufanya naye kazi.

Ameeleza kuwa,kwasasa anapata shida kuwahudumia watoto wake hasa kulipa ada na mahitaji muhimu kwao baada ya kipato chake kushuka kutokana na kuidai Kampuni ya skywards kiasi kikubwa cha fedha .
Amesema pamoja na wao kushikiliwa mitaji yao kwa muda wa miaka miwili sasa,lakini pia serikali inapoteza Kodi kwenye hiyo fedha maana wangekuwa wamelipwa na wao wangeweza kulipa Kodi.

Aidha Joyce Edward ambaye amejitambulisha Kama Mke wa mfanyabiashara Karim Chasama amesema walikopesha bidhaa ya Mabati kwa kampuni hiyo wakati inajenga chuo cha VETA eneo la mtaa wa Mine Mpya mjini Geita.

Amesema kuwa wanadai zaidi ya Milioni 51 ambazo hadi Sasa hazijalipwa na kuwasababishia usumbufu wa kudaiwa na TRA na mabenki na kuwa na hali ngumu kimaisha.

Kampuni ya Skywards company limited inatajwa kuingia Mkataba wa ujenzi wa chuo ufundi stadi mjini Geita katika eneo la mtaa Mine Mpya chini ya VETA na baada ya Waziri Ndalichako kutembelea chuo hicho na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi aliagiza uchunguzi ufanyike.

Siku chache baada ya maelekezo ya waziri Ndalichako Veta ilitangaza kuvunja mkataba na kampuni hiyo jambo ambalo linatajwa kusababisha mkandarasi huyo kuondoka eneo la mradi bila kulipa wafanyabiashara hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news