Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaongoza viongozi mbalimbali wa Serikali katika mapokezi ya mwili wa Hayati Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ulipowsili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza ukitokea jijini Zanzibar, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Mwanza).
Mwili huo umewasili majira ya saa 1:31 asubuhi kwa ndege na kuondolewa uwanjani kwa gari maalum hapo majira ya saa 2:08 kuelekea kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ambako shughuli ya kuagwa na kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo ilifanyika ambapo kabla mwili huo ulishushwa na maofisa wa jeshi wenye vyeo vya Kanali na kuuingiza kwenye gari majira ya saa 2:03.
Wakati wa mapokezi hayo ya mwili wa Hayati Rais Magufuli,mbali na Waziri Mkuu, alikuwepo Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Hemed Seleman Abdallah,Waziri wa Mambo ya Nje, Ushikiano wa Afrika wa Mashariki Kikanda na Kimataifa, Profesa Paramagamba Kabudi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mali za CCM, Christopher Gachuma.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiambatana na Wakuu wa Mikoa ya Mara,Adam Malima,Zainabu Terack wa Shinyanga na Brigedia Jenerali,Michael Gaguti wa Kagera na viongozi wengi wa Chama na Serikali.
Mara baada ya mwili huo kuondolewa uwanjani wa ndege,vilio vimesikika kutoka kwa akina mama waliojitokeza kuupokea wakiwa wamejipanga kando ya barabara ya Makongoro kutoka uwanja wa Ndege kuelekea CCM Kirumba.
Gari lililobeba jeneza la mwili wa Rais Magufuli, ulisindikizwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi ambao waliungana na wananchi kuusindikiza kwa kukikimbia pembeni mwa gari hilo.
Msafara huo ulipita maeneo ya Ilemela, Sabasaba, Iloganzala, Pasiansi,Nyamanoro, Seleman Nassoro ambako aliwahi kuishi akiwa Waziri wa Ujenzi, Kona ya Bwiru,Gana kupitia barabara ya Furahisha hadi CCM Kirumba.
Wakati wote kwenye maeneo mwili huo ulikopita,wananchi walijipanga kando ya barabara huku wengi wakiangua vilio mara baada ya kuona msafara wa magari likiwemo lililobeba jeneza la mwili wake ambako eneo la Seleman Nassoro msafara huo ulisimama kwa dakika moja ili kutoa fursa kwa majirani zake kutoa heshima za mwisho.
Wananchi hasa akina mama wametandika kanga barabarani kuonyesha heshima kwa mwili wa Rais Magufuli, huku vijana wakiimba Magufuli Jeshi,Jeshi,Magufuli Jeshi huku wengine wakiwa wanapunga matawi ya miti baadhi wakiwa wamejipanga kando mwa barabara maeneo yote mwili huo ulikopita.
Aidha,msafara huo kutoka uwanja wa ndege ulisindikizwa na chopa za JWTZ na polisi, kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa huku Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kallli akitembea kwa na kukimbia kutoka uwanja wa ndege muda wote akiwa pembeni mwa gari lililoubeba mwili wa Hayati Rais Magufuli.
Mwili huo uliingia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba majira ya saa 3:17 na kusababisha vilio kuibuka zaidi kutoka kwa maelefu ya waombolezaji ambapo ulizungushwa mara moja kwenye uwanja huo kabla ya kushushwa na maoifa wa JWTZ wenye vyeo vya Kanali na kuingizwa kwenye banda maalum lililotumika kuaga ambpo majira ya saa 3:32 ulipigwa wimbo wa Taifa ukifuatiwa na wimbo wa Afrika Mashariki.
Baadaye saa 3:37 ilifuatiwa sala iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Askofu Renatus Nkwande kisha dua maalum iliyosomwa na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikh Hasan Musa Kabeke kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza.
Wengine ni viongozi Kanisa la AIC Askofu Emmanuel Sinteme na Askofu Dk. Charles Sekelwa wa Umoja wa Makanisa ya Pentekoste pamoja na Sheikh wa Msikiti wa Jay Swamminarayyan.
Wananchi wa Jiji la Mwanza wameweka historia kwa umati uliojitokeza kuupokea mwili wa Hayati Rais Magufuli, kwa namna walionyesha mapenzi makubwa na jinsi walivyoupokea na kuusidikiza hadi CCM Kirumba.
Alionyesha kuwa Rais aliyependwa na wananchi wake, laiti leo angekuwa hai akaona jinsi Watanzania walivyojitokeza kuuaga mwili wake baada ya kifo angefarijika huko kaburini
Tags
Habari