Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu), Andrew Massawe, ameziagiza taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo
kuvihusisha vyombo vya sheria katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta
usawa na uwajibikaji miongoni mwa taasisi husika na wadau wao, anaripoti
Mwandishi DIRAMAKINI.

Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
(OSHA), Idara ya Kazi, Tume ya Uamuzi na Usuluhishi (CMA), Mfuko wa
Hifadhi kwa Jamii wa Sekta Binafsi (NSSF), Mfuko wa Hifadhi kwa Jamii wa
Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Maagizo
hayo ameyatoa alipofunga semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali
pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ambayo ilitolewa na OSHA kwa Mawakili wa
Serikali chini ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP).

Katibu Mkuu huyo amesema Taasisi hizo zinapaswa kushirikiana na
vyombo hivyo vya dola kwa kutoa mafunzo kwa watumishi mbali mbali katika
vyombo hivyo ili kuleta uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa sheria
mbali mbali ambazo utekelezaji wake unasimamiwa na Taasisi hizo.
“Kunakuwa
na ugumu endapo kila Taasisi itapambana peke yake katika kushughulikiwa
masuala mbali mbali ya kisheria yanayoihusu hivyo ili kuleta ufanisi
katika utekelezaji wa sheria zenu ni muhimu sana kuvishirikisha vyombo
vya kisheria vya serikali ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa
Serikali (DPP), Wakili wa Serikali (Solicitor General), Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (Attorney General) na Jeshi la Polisi,” alieleza Katibu
Mkuu huyo.

Akifungua semina hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija
Mwenda, amesema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja baina
ya OSHA na Mawakili wa Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria
husika.
“Tunaamini kwamba kupitia mafunzo haya ya leo mtapata
kufahamu kwa undani dhumuni kuu la Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama
Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na pia namna ambavyo OSHA inasimamia
utekelezaji wa sheria husika na hivyo tutaweza kushirikiana vizuri
katika kuhakikisha kwamba sheria inatekelezwa ipasavyo,” alisema Mwenda.

Baadhi ya Mawakili wa Serikali walioshiriki katika semina wakiwemo Adolf Verandumi, Mkunde Mshanga na Esther Chale wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa kuandaa mafunzo hayo. Aidha, wameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wamejifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kusimamia mashauri mbali mbali yanayohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
“Kimsingi semina hii imetufungua na kutupatia mwanga katika changamoto ambazo tumekuwa tukikumbana nazo katika kushughulikia mashauri yanayohusu Usalama na Afya mahali pa kazi. Kwahiyo, tunashauri semina kama hizi ziweze kuwa endelevu na zifanyike pia kwa makundi mbali mbali na wadau tofauti tofauti,” alieleza Esther Chale ambaye ni Wakili wa Serikali.
Tags
Habari