Makamu wa Rais Zimbabwe, Kembo Mohadi (71) amejiuzulu Machi Mosi, Mwaka huu kutokana na madai ya kashfa ya ngono.
Vyombo vya habari vya Zimbabwe vimeripoti kuhusu kashfa hiyo tangu Februari, 2021 kufuatia sauti ya mazungumzo ya simu yanayodaiwa kuwa ni ya Mohadi akiomba kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wake za watu ikiwa ni pamoja na msaidizi katika ofisi yake.
Taarifa ya kwanza iliyochapishwa katika mtandao wa ZimLive inasikika sauti ya mwanaume akiomba kufanya mapenzi ofisini.
“Ninajiuzulu nafasi yangu ya makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe kuanzia sasa,” amesema Mohadi katika barua yake iliyotumwa kwenye ukurasa wa Twitter wa Wizara ya Habari.
“Si kwa sababu ya udhaifu bali kwa sababu ya kuiheshimu ofisi ili isihusishwe au kuchafuliwa na matendo yanayohusishwa na changamoto za mtu. Nimekuwa katika maombi ya kutafakari moyoni mwangu nikaona nahitaji kuwa na nafasi ya kushughulikia matatizo yangu nje ya Serikali.”
Alikanusha kuhusika na kashfa hiyo amesema, “nilikuwa mwathiriwa wa taarifa feki, sauti ya kughushi na kashfa ya kutengeneza na njama za kisiasa.”
Jacob Ngarivhume, kiongozi wa upinzani amesema uamuzi huo wa Mohadi ni ushahidi wa madudu ya chama cha Zanu-PF.