Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa wizara zote

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha inaviimarisha vitengo vyao vya habari ili kurahisisha mfumo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi “Sema na Rais Mwinyi” unatekelezeka, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia Mukhtasari wa Taarifa ya Utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha, ikiwasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais ) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 3, 2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi pamoja na watendaji wa ofisi hiyo, ikiwa ni mkutano kwa ajili ya kuripoti utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Rais kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha.

Katika maelezo yake hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba kuna haja ya kuhakikisha vitengo hivyo vya habari katika wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, vinaimarishwa ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa ya mfumo huo yanafikiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi, wakati wa kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati wa kuwaapisha, mkutano huo umefanyika katiuka ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Katika mkutano huo ambapo Makamu wa Pili alihudhuria, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni vyema pale wananchi watakapoanza kutoa malalamiko yao wakawa wanapata majibu kwa uhakika kutoka taasisi husika.

Amesisitiza haja ya kuwepo kwa mtu maalum atakayehusika na kazi hiyo katika vitengo hivyo wizarani ambaye atakuwa anaripoti na kupeleka sehemu husika malalamiko hayo na hatimaye kuweza kupatiwa majibu kwa haraka. 

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza umuhimu wa utekelezaji wa mfumo huo ambao utawasaidia wananchi na kusisitiza kwamba hatua zote zinazoendelea yeye atakuwa akiziona.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Ndg.Thabit Idarous Faina, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati wa kuwaapisha, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi, Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu).

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alipongeza juhudi zilizochukuliwa na uongozi wa wizara hiyo katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa na kusisitiza haja ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo.

Rais Dkt. Mwinyi pia, alieleza umuhimu wa Mifuko ya Uwezeshaji kuwa pamoja hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwarahisishia walengwa kunufaika kirahisi.

Pia, Rais Dkt. Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba vikao hivyo vitakuwa endelevu kwa lengo la kuweza kupata mafanikio na changamoto ambapo hatimae kutafuta ufumbuzi wa utatuzi wa changamoto hizo kwa azma ya kupata ufanisi mzur zaidi.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais , Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dkt. Khalid Mohamed Salum alianza kwa kutoa pole kwa Rais kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea hivi karibuni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-3-2021 na (kushoto kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu).

Waziri Khalid Mohamed Salum alimueleza Rais Dkt.Mwinyi historia ya kuanzishwa kwa ofisi hiyo huku akieleza kwamba ofisi hiyo ni kiungo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Khalid alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua zilizochukuliwa na Ofisi hiyo katika utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu mara baada ya kuapishwa Novemba 21, 2020 na Januari 25,2021.

Aidha, alieleza kwamba ofisi hiyo ndiyo mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Serikali, hivyo kama zilivyo Wizara na Taasisi nyingine inahitaji mazingira mazuri ya kazi na nyenzo za uhakika ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa mkutano huo wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa namna alivyoanza na kuendelea kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kumpongeza Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa miongozo yake na ushauri anaowapa.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alieleza haja ya kuwepo elimu zaidi kwa wananchi katika kuhakikisha malengo ya mfumo wa “Sema na Rais Mwinyi” yanafikiwa kwani mfumo huo umepokewa vizuri.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Thabit Idarous Faina alieleza jinsi Wizara hiyo ilivyotekeleza maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati alipowaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu ambapo miongoni mwa utekelezaji huo ni pamoja na Waziri kutembelea Taasisi zilizokuwemo katika Ofisi hiyo, kulipa madeni ya Serikali pamoja na mambo mengineyo.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya miradi 12 imeibuliwa na kuwasilishwa Tume ya Mipango ambayo inaitarajiwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/26 baada ya kuidhinishwa katika ngazi husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news