Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kwamba mbali ya ibada ya sala tano ni vyema misikiti ikafanya kazi ya kushughulikia matatizo ya jamii, anaripoti Mwandishi Maalum DIRAMAKINI (Pemba).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Mwakilishi wa Mfadhili wa ujenzi wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale Pemba, Bw. Humoud Mohammed alipowasili katika viwanja vya Msikiti huo kwa ajili ya ufunguzi uliofanyika leo 12-3-2021. Kabla ya Sala ya Ijumaa.(Picha na Ikulu)
Alhaj Dkt.Mwinyi alitoa rai hiyo leo Machi 12, 2021 wakati akiufungua Msikiti Taqwaa ulioko Gombani ya kale Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuitumia misikiti kwa kutatua changamoto kadhaa za kijamii.
Katika hotuba yake Alhaj Dkt. Mwinyi alieleza kwamba, bado misikiti haijatumika ipasavyo na walio wengi wanadhani misikiti ni kwa ajili ya sala tano pekee, hali ambayo iwapo misikiti itatumika vizuri itasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kwa ajili ya ufunguzi wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale Pemba Wilaya ya Chakechake (kulia kwa Rais) Mwakilishi wa Mfadhili wa Ujenzi wa Msikiti huo Bw. Humoud Mohammed na Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Mahmoud Mussa Wadi.(Picha na Ikulu).
Amesema kwamba ni vyema misikiti ukiwemo huo alioufungua iwe na idara mbali mbali zitakazojadili changamoto za jamii ikiwemo kuwasaidia wajane sambamba na suala zima la udhalilishaji ili mambo hayo yaondoke katika jamii.
Hivyo, Dkt. Mwinyi amesema, haitakuwa busara kuona mskiti huo uliojengwa kwa gharama kubwa, usitumike kupanga mipango na mikakati mbalimbali ya kuisadia jamii iliyopo katika eneo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiondoa kipazia kwa ajili ya ufunguzi wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale Pemba akiwa na Mwakilishi wa Mfadhili wa ujenzi huo Bw. Homoud Mohammed,hafla hiyo imefanyika leo 12-3-2021.(Picha na Ikulu).
“Katika karne hii tuliyonayo, bado miskiti haijatumika na tuliowengi tukishamaliza kusali sala tano, ndio kazi imekwisha, kumbe tunamakundi kama ya wajane ambayo yanachangamoto mbalimbali,’’ameeleza.
Akizumgumzia hali duni ya walimu wa madrasa na maimamu katika misikiti Alhaj Dkt. Mwinyi ameitaka jamiii kukaa pamoja kuangalia ni vipi wanawasaidia.
Aidha, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha ahadi alizoziweka anazitekeleza hatua kwa hatua.
Alieleza kuwa, anaelewa vyema changamoto zilizomo ndani ya jamii mfano kwenye sekta ya miundombinu ya barabara, afya, maji safi na salama pamoja na elimu, hivyo atahakikisha anaimarisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na kuzungumza na Waumini wa Kiislam wa Masjid Taqwa Gombani baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa na kuufungua rasmi Msikiti huo leo 12-3-2021.(Picha na Ikulu).
Aliwataka waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wengine kuendelea kumuombea dua kila wakati, ili afanikishe malengo na kutekeleza ahadi zake alizowaahidi wananchi hao huku akimpongeza mfadhili wa msikiti huo.
“Naomba niwakumbushe kuwa, nakumbuka kuwa nna ahadi kwenu ambazo niliwaahidi, hivyo malengo na dhamira nnayo, hivyo niombeeni dua ili nifanikishea hayo,’ ’alieleza Alhaj Dk. Mwinyi.
Kuhusu amani na utulivu uliopo nchini, Alhaj Dk. Miwnyi alisema kuwa Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha amani na umoja unadumu ili wananchi wafanye shughuli zao za maendeleo.
Alisema, ataendelea kusisitiza jambo hilo kila anapokutana na wananchi, kwani ndio msingi wa kila jambo, katika nchi na jamii kwa ujumla.
“Hata Khatibu wetu wakati anatupa daawa, alieleza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwetu na kutumia aya mbali mbali, sasa na mimi nitaendelea kulisisiti jambo hilo,’’alifafanua.
Akizungumzia hofu waliyokuwa nayo baadhi ya wananchi wa Zanzibar mara baada ya kifo cha Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad Febuari 17, juu ya kuendelezwa maridhiano, Alhaj Dk. Mwinyi aliwatoa hofu wananchi.
Alisema kwa bahati nzuri amepatikana Makamu wa kwanza wa Rais ambaye tayari ameshakaa nae na kumuahidi kuendeleza maridhiano na umoja wa Wazanzibari kama ilivyo azma ya Serikali iliyopo.
Mapema Katibu wa Mufti wa Zanzibar sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema kuna malipo makubwa kwa aliyejenga msikiti, ikiwa ni pamoja na kuwa na makaazi kwenye pepo ya Allah.
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akizungumza katika hafla ya Ufunguzi wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale kabla kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na Wananchi na Waumini wa Kiislam katika hafla hiyo.(Picha na Ikulu).
Alisema kilichobakia sasa baada waumini wa dini ya kiislamu wa Gombani kujengewa msikiti huo, ni kuutunza na kuanzisha idara zitakazoijenga jamii.
“Lazima kuwe na Idara ambazo zitatunza mskiti, kushughulikia suala la taaluma pamoja na kuwa na vikao vya kutatua changamoto kadhaa zilizomo ndani ya jamii,’’alieleza.
Akizungumza kwa niaba ya mfadhili wa msikiti huo, Sheikh Mohamed Suleiman Khalfan, alisema wameamua kuujenga msikiti huo, baada ya uliyokuwepo kuwa na nafasi finyu kwa waislamu.
“Leo tumefurahishwa mno na ujio wa Rais wa Zanzibar katika ufunguzi wetu, maana alikuwa na uwezo wa kuwatuma wasaidizi wake, hii inaonesha imani yake kwenye mambo ya kheiri,’’alieleza.
Akisoma risala ya wauimini wa dini ya kiislamu wa Gombani pamoja na wananchi wengine, ustadh Hamad Mussa Rashid alisema jina la ‘Taqwaa’ la mskiti huo liliasisiwa na Mufti wa sasa Sheikh Saleh Omar Qaabi tokea mwaka 1988.
Alisema wakati huo palikuwa na msikiti mdogo, ambao baadae waliomba ufadhili ili kujengewa mkubwa, kutokana na wakati huo kuzidiwa na waumini.
“Leo kwetu wananchi na waumini wa dini ya kiislamu wenzetu wa hapa Gombani na Chake chake, tumefarajika mno kuona tunahamia kwenye msikiti ambao umeshaondosha tatizo la sehemu ya kufanyia ibada,’’alieleza.
Alisema msikiti huo ambao unatarajiwa kuwa na ghorofa mbili, juu na ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya ibada ya swala na ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya madrassa ya watoto wao.
Akisoma hutuba mbili ya swala ya Ijumaa sheikh Khalifa Mrisho Omar, alisema rais Alhajj Dk. Mwinyi amekuwa na sifa nzuri ya kujali shida na matatizo ya wananchi wake.
“Kiongozi wetu huyu amekuwa na sifa za kipekee, kwa kule kuwa karibu na wananchi na kujali na kufuatilia kwa karibu changamoto zetu,’’alieleza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Viongozi na Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Msikiti huo wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale Pemba.(Picha na Ikulu).
Ujenzi wa masjid taqwaa ambao ulianza Febuari 2, mwaka 2019 kwenye eneo lake la chini ambalo limejengawa sasa, unauwezo wa kusaliwa na waumini 840 wanawake na wanaume, na umegharimu shilingi milioni 600.
Hata hivyo, ukimaliza ghorofa zote mbili, utakuwa na uwezo wa kusaliwa na waumini 2000, huku Rais wa Zanzibar akiahidi nae kuchangia katika uendelezaji wa ujenzi wa mskiti huo.