
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 28 Machi, 2021 amepokea taarifa za mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Hafla ya kupokea taarifa hizo imefanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na viongozi wakuu wa taasisi na idara za Serikali.
LIVE TAZAMA HAPA CHINI
Mhe. Rais Samia ameipongeza ofisi ya CAG na TAKUKURU kwa kazi za ukaguzi na uchunguzi zilizofanywa katika mwaka 2019/20. Ameiagiza ofisi ya CAG kuongeza wataalamu wa ukaguzi ili waweze kukagua mashirika mengi zaidi na miradi mingi zaidi hususani iliyopo mikoani ambayo maendeleo yake hayaridhishi.
Kutokana na taarifa ya CAG kuonesha kuwa kuna kusuasua kwa utekelezaji wa mapendekezo juu ya usimamizi wa hesabu za Serikali na hali isiyoridhisha ya mashirika na taasisi za Serikali, Mhe. Rais Samia ameahidi kuongeza msukumo katika utekelezaji wa mapendekezo hayo na kuchukua hatua za haraka dhidi ya mashirika na taasisi ambazo zimetajwa kufanya vibaya kutokana na wizi na upotevu wa fedha za umma.




Ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko kufuatia taarifa za kuwepo upotevu wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 3.6 na ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi katika mamlaka hiyo.
Mhe. Rais Samia amemuagiza CAG Charles Kichere kufanya ukaguzi wa fedha zote zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kati ya mwezi Januari na Machi, 2021.
Ameitaka Ofisi ya CAG na TAKUKURU kushirikiana kuweka sawa mifumo ya fedha inayotumiwa na hazina ili kuondokana na changamoto na athari za kuwepo mifumo mingi tena isiyowasiliana na ambayo inasababisha upotevu mkubwa wa fedha.

jijini Dodoma leo Jumapili Machi 28, 2021


28, 2021.






Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Jumapili Machi 28, 2021.
Kuhusu mashirika yasiyofanya vizuri amemtaka CAG kutomung’unya maneno akisema “mashirika yasiyofanya vizuri, naomba sana CAG ulimi wako usiwe na utata, kama kuna shirika halifanyi vizuri tuambie hili halifanyi vizuri, kama bodi haisimami vizuri tuambie bodi hii haisimami vizuri, kwa sababu tutakaposema mapungufu ndipo tutakapoweza kurekebisha na kufanya vizuri zaidi, tukinyamaziana na kuficha sura hatutarekebisha na tutawaumiza wananchi, naomba sana ripoti yako iwe wazi zaidi, utakaponiletea ukaguzi wa mashirika naomba uwe wazi zaidi ili tujue tunachukua hatua gani”.
Kwa upande wa TAKUKURU, Mhe. Rais Samia ameitaka taasisi hiyo kuongeza juhudi zaidi kwa kuharakisha kufikisha Mahakamani kesi za rushwa na ufisadi, kuachana na kesi ambazo hazina msingi wa kushinda na ameitaka taasisi hiyo kujielekeza zaidi katika masuala yanayohusiana na rushwa na yale yanayopaswa kufanywa na vyombo vingine viachiwe vyombo husika.
Amehimiza uadilifu kwa watumishi wa TAKUKURU ambao wamekuwa wakiwafichua mashahidi na watoa taarifa na pia ametaka taasisi hiyo ipanue uwigo wa kufuatilia vitendo vya rushwa ikiwemo uvujaji wa mitihani, kuboresha mifumo yake ya kukabiliana na rushwa na ufisadi na ishirikiane na taasisi nyingine katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa.
Mhe. Rais Samia amewahakikishia Watanzania kuwa atasimama imara kulinda makusanyo na matumizi ya fedha za Serikali pamoja na vita dhidi ya rushwa.
Katika taarifa yake CAG Charles Kichere amesema katika mwaka 2019/20 ofisi yake imetoa jumla ya hati 900 za ukaguzi (zikiwemo 243 za Serikali Kuu, 185 Serikali za Mitaa, 165 za Mashirika ya Umma, 290 za miradi na 17 vyama vya siasa) ambapo 800 (89%) zinaridhisha, 81 zina mashaka (9%), 10 mbaya (1%) na hati 9 alishindwa kutoa maoni.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Jen. John Mbungo amesema katika mwaka 2019/20 taasisi hiyo ilifanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita ilipotekeleza majukumu yake kwa asilimia 88.1 ongezeko ambalo limetokana na kukamilisha uchunguzi kwa majalada 1,079 ikilinganishwa na majalada 911 ya mwaka uliopita.
Tags
Habari