Rhobi Samwelly ataja faida za kuwekeza elimu kwa watoto wa kike

NA FRESHA KINASA

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT), Rhobi Samwelly amesema jamii inawajibu wa kuendelea kuwathamini Wwnawake pamoja na kutambua mchango wao katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na hivyo iwekeze nguvu kuwasomesha watoto wa kike kwa manufaa ya Taifa kwa siku za usoni.
Sehemu ya Wasichana Kutoka kituo cha Nyumba Salama Mugumu kinachomilikiwa na Shirika la (HGWT). Nyuma yao ni Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbalibali wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Nurdin Babu katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani. (Picha na FRESHA KINASA).

Rhobi ambaye amewahi kutunukiwa Tuzo ya Malkia wa Nguvu kutokana na juhudi zake za kupigania haki za binadamu na kupinga ukatili wa kijinsia amesema, iwapo jamii itaweka msukumo thabiti katika kuwathamini wanawake na kutambua mchango wao, hapatakuwa na uzembe katika kuwaandaa kuja kuwa viongozi katika jamii, tasisi na hata Taifa kwani kila mmoja atashiriki kikamilifu kuwatengenezea mazingira wezeshi mabinti kuzitimiza ndoto zao.

Ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo katika Wilaya ya Serengeti yalifanyika Kijiji cha Mbalibali na kuhudhuria na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi zinazopingana na ukatili, wazee wa kimila, wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa wilaya hiyo Nurdin Babu aliyekuwa Mgeni rasmi.
Rhobi Samwelly,Mkurugenzi wa HGWT. 

Rhobi aliitaka jamii kupata funzo kwa viongozi wakubwa wa Serikali ambao ni wanawake akiwemo Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Tanzania pamoja na Mawaziri wengine ambao ni Wanawake na wanatoa mchango mkubwa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa akasema hatua waliyo nayo ni matunda ya elimu na hivyo akahimiza jamii kuwasomesha watoto wa kike bila kuwabagua.

Aliiomba jamii kuachana na mila kandamizi dhidi ya watoto wa kike ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, kurithi wake, utumikishwaji Wwtoto akasisitiza wananchi kusomesha Mabinti kwani kufanya hinyo ni kuwapa urithi pekee na dira ya maisha yao badala ya kuwaozesha kwa nia ya kupata mifugo (ng'ombe) kitu ambacho hakina faida.
Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti. (Picha na FRESHA KINASA).

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu mbali na kupongeza juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika kupambana na ukatili wilayani humo na Mkoa wa Mara kwa ujumla, aliwaomba Wazee wa Kimila kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni kwani wananguvu ya ushawishi na kwamba wakikemea vitendo hivyo Jamii itawasikiliza na kutekeleza maelekezo yao.

Aidha, Mhe. Babu aliahidi kuyapa ushirikiano mashirika mbalimbali wilayani humo yanayofanya kazi ya kupinga ukatili wa kijinsia kwani dhamira ya Serikali alisema ni kuona ukeketaji unamalizika na kwamba Watoto wa kike wanasoma kwani serikali inatoa elimu bila malipo kusudi kila Mtoto apate fursa ya elimu kwa ajili ya kuiandaa kesho yake yenye kung'ara.

Katika hatua nyingine, Mhe. Babu aliwataka wazazi kuondokana na kasumba ya kuwazuia watoto kwenda shule ili wakachunge mifugo, ambapo alibainisha kwamba mtoto atakayebainika akichunga hajahudhuria shuleni adhabu kali itatolewa kwa mzazi kwani kufanya hivyo ni kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuandaa Taifa la wasomi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news