SERIKALI YAONYA WANAONG'OA ALAMA ZA UPIMAJI ARDHI

Serikali imewaonya wamiliki wote wa ardhi wanaoharibu, kung'oa na kuhamisha alama za upimaji ardhi (Beacons) na kueleza kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipa faini ya shilingi 750, 000 au kifungo cha mwaka mmoja jela,anaripoti Munir Shemweta (WANMM).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupitia kitengo chake cha Mawasiliano Serikalini ni kosa kisheria kufanya shughuli yoyote inayoweza kusababisha kuharibu, kung'oa au kuhamisha alama za upimaji.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imebaini uwepo baadhi ya wananchi wanaoharibu, kung'oa na kuhamisha alama za upimaji na kubainisha kwamba, kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Kupitia taarifa yake Wizara ya Ardhi imeeleza kuwa, kutokana na kukithiri vitendo hivyo inawakumbusha wananchi wote kuwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu, kung'oa, kuhamisha au kufanya shughuli inayoweza kuharibu alama za upimaji ardhi atakuwa ametenda kosa la jinai na atawajibika kulipa faini shilingi 750,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela au adhabu zote kwa pamoja.

Wizara ya Ardhi imewaasa wananchi wote kutojihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa vinarudisha nyuma jitihada za serikali za kuongeza usalama wa miliki ardhi kwa wananchi.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikipanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa lengo la kuongeza usalama wa miliki za ardhi kwa wananchi na maeneo yote yaliyopangwa na kupimwa yamewekewa alama za upimaji ardhini ( Beacons) kwa mujibu wa sheria ya upimaji ardhi sura ya 324.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news