Shule ya Sekondari maalum kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini ya Patandi iliyopo Jijini Arusha, imeanza kupokea wanafunzi baada ya serikali kukamilisha ujenzi wake kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Arusha).
Akihojiwa na waandishi wa Habari, Mkuu wa Shule hiyo Janeth Mollel, amesema hadi sasa wanafunzi 143 ambapo kati yao 93 ni wenye ulemavu wameripoti kuanza masomo yao wiki mbili zilizopita.
Amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo umegharimu kiasi cha skilingi bilioni 3.6 na ni shule ya kwanza ya serikali nchini kujengwa kwa ajili ya watoto wenye ulemavu mbalimbali.
“Hii shule inachukua watoto hawa wenye mahitaji maalum nchi nzima, tunashukuru serikali chini ya Rais John Magufuli kwa kuona umuhimu wa kujenga shule hii, ambayo ni ya kipekee Tanzania nzima na inawezekana pia Afrika Mashariki,”amesema.
Amesema shule hiyo upekee wake inachukua wanafunzi wa aina zote ni elimu jumuishi ambapo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa bweni na kutwa 600 huku uwezo wake wa mabweni ni kuchukua wanafunzi wa 416.
“Kuna watoto wenye ulemavu wa aina zote wanasoma hapa, watoto wasiosikia na wanaotumia viti mwendo, miundombinu ya shule hii imezingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu, kuna vyumba maalum kwa ajili ya wanafunzi ambao wanaulemavu mkubwa wa viungo, ambapo vyumba hivyo vina vyoo ndani,”amesema.
Amesema walimu wao ni waliosomea kufundisha watoto wa aina hiyo na wanafunzi wasio na mahitaji maalum ili kushirikana nao na kujiona hawajatengwa na jamii.
“Wanakula na kucheza na walimu, kwa ujumla watoto wanafurahia maisha ya hapa Patandi, nitoe rai kwa jamii kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miundombinu hii,”amefafanua.
Molell ametoa wito kwa jamii kuacha kuwaficha watoto hao ili wasome wafikie ndoto zao.
Ameiomba serikali kujenga shule nyingine ya mfano za aina hiyo kwenye maeneo mengine ili wanafunzi waondokane na kusafiri umbali mrefu.
“Kwa mfano nina mtoto anaitwa Rebeca anatokea Kusulu Kigoma, sasa ili kuondokana na tatizo la kusafiri umbali mrefu ni vizuri ikaona umuhimu wa kujenga shule kama hii kwenye maeneo hayo,”amesema.
Naye, Mmoja wa wanafunzi hao, Nurueli Thomas, alisema mazingira ya shule hiyo yanaendana na hali halisi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Tunashukuru serikali kwa kujenga miundombinu hii mizuri na ya kuvutia, walimu wanafundisha vizuri, miundombinu hii itasaidia kusoma vizuri na kufikia ndoto zetu, tunaahidi serikali hatutaiangusha tutafaulu vizuri kwenye mtihani wa kidato cha nne,”amesema.
Tags
Habari
Yes shule ni nzuri Sana hasa kwa kutimiza malengo na kauli mbiu ya mpango mkakati wa elimu jumuishi inchini
ReplyDelete