Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Magufuli amefariki dunia leo Machi 17, 2021 akiwa katika matibabu, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).
Taarifa rasmi iliyotolewa kwa umma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) leo usiku Machi 17, 2021 saa 5 usiku imeeeza kuwa Rais Magufuli amefariki dunia leo majira ya saa 12 jioni kwa maradhi ya Moyo akiwa katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli alilazwa tarehe 6 Machi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la moyo wa mfumo wa umeme ambalo limekuwa likimkabili kwa takirbani miaka 10. Nchi itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti.
"Tumempoteza Kiongozi wetu Shupavu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, alilazwa tarehe 6 Machi mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.
“Rais Magufuli amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena, alilazwa Machi 6,2021 katika Hospitali ya Jakaya Kikwete na kuruhusiwa Machi 7 na kuendelea na majukumu yake.
“Machi 14 alijisikia vibaya na akarudi Hospitali ya Mzena ambapo aliendelea na matibabu hadi umauti unamkuta, Nchi yetu itakuwa na maombolezo ya siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti,"amesema Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu.