TCRA yatangaza neema kwa watumiaji wa simu za mikononi Tanzania

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mwongozo wa kanuni ndogo 12 ambazo zitasaidia kutatua kero za watumiaji wa huduma na kuongeza ustawi wa sekta ya mawasiliano, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).

Mkurungezi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba.

Hatua hiyo imekuja baada ya TCRA kupokea jumla ya maoni 3,278 ya malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ikijumuisha watumiaji, watoa huduma,Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Utekelezaji wa kanuni hizo unatarajia kuanza Aprili 2, mwaka huu na kufanikiwa kujibu mambo mbalimbali yanalolalamikiwa na wateja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 2, 2021, Mkurungezi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema kwa kuzingatia maoni na ushauri wa wadau TCRA imeweza kuandaa kanuni hizo ambazo zitasaidia kutatua kero.

Amesema, baadhi ya mambo yaliopo katika kanuni hizo ni pamoja na mtoa huduma hatatoa huduma za vifurushi bila kibali cha mamlaka.

Mhandisi Kilaba amesema, mtoa huduma anapaswa kuhakikisha kwamba bei za vifurushi zinazingatia bei husika ya chini na ya juu zilizowekwa na mamlaka, pamoja na kutumia lugha rahisi na vigezo na masharti yaliyo wazi kuhusu vifurushi vinavyotolewa.

Amesema, vifurushi vinavyotolewa kwa mtumiaji havitaondolewa, havitarekebishwa au kubadilishwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa, mtoa huduma ataweka utaratibu au mfumo wa kumuwezesha mtumiaji mwingine ndani ya mtandao wake kwa masharti.

"Mtumiaji wa huduma ataweza kuhamisha kifurushi cha MB kwa watumiaji wasiozidi wawili, lakini pia mtumiaji aliyeamishiwa unit za kifurushi hataruhusiwa kumhamishia mtumiaji mwingine uniti hizo au sehemu za uniti hizo,"amesema.

Amesema, mtoa huduma hataruhusiwa kupunguza kasi ya data kwenye kifurushi cha mteja ndani ya muda wa kifurushi husika, mtoa huduma hatafanya promosheni zaidi ya tatu au kutoa ofa maalum zaidi ya tatu kwa wakati mmoja kupitia huduma za sauti, sms na data.

Mhandisi Kilaba amesema, kanuni hizo zitakapoanza kutumika zitasaidia kujibu malalamiko mengi ya wateja kwa sasa na kusisistiza watumiaji kuendelea kufuatilia mabadiliko hayo kwa umakini na kwa mtazamo chanya.

"Kupitia kanuni hizi zitaboreeha huduma za vifurushi kutokana na maoni ya wengi kuwa vifurushi vimekuwa vikiwasaidia,"amesema.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Kilaba amewataka watanzania kuendeleza kupambana na masuala ya utapeli mtandaoni na kuwataka kuendelea kusoma mwongozo wa TCRA kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano.

"Usikubali kutapeliwa kwa kutekeleza maelekezo yanayohusu mhamala wowote wa kifedha katika simu yako, kwa kupigiwa simu na mtu yeyote anayejifanya mfanyakazi wa kampuni yoyote ya simu au wakala wake,"amesema Mhandisi Kilaba.

Pia amesema, ikitokea mtumiaji wa simu amepigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wowote wa kitapeli asiutekeleze badala yake autume ujumbe huo kwa namba 15040 na namba iliyoutuma ujumbe hiyo kwa ajili ya kuchukua hatua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news