TSC yaanza maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa kutembelea vituo vya watoto yatima

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wameanza maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa kutembelea vituo vya watoto yatima vya Nyumba ya Matumaini na Cheshire Home vilivyopo eneo la Miyuji jijini Dodoma,anaripoti Adili Mhina (TSC).
Afisa Utumishi kutoka TSC, Judith Mtalai akiongea na watoto wa kituo cha watoto yatima cha Nyumba ya Matumani kilichopo Miyuji, Dodoma wakati watumishi wa TSC walipotembelea kituo hicho na kutoa zawadi mbalimbali.

Ziara hiyo ilifanyika Machi 3, 2021 iliratibiwa na wanawake ambao ni wafanyakazi wa tume kwa lengo la kuwajulia hali watoto wa vituo hivyo pamoja na kuwapatia zawadi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake ambayo hufanyika Machi 8.

Kiongozi wa msafara huo ambaye pia ni Afisa Utumishi kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu TSC, Judith Mtalai alieleza kuwa akinamama hao waliamua kuchangishana pesa ili waweze kununua zawadi kidogo kwa ajili ya watoto.

“Tuliona kuwa badala ya kusubiri tarehe 8 Machi na kwenda uwanjani kufurahia siku ya wanawake, ni bora tuanze kwa kuwajali watoto wetu ili nao wajisikie kuwa tupo wazazi tunaowapenda na kuwajali wakati,”amesema Mtalai.

Alieleza kuwa zipo changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto katika vituo mbalimbali, hivyo watoto hao wanahitaji kuwekwa karibu na jamii kwa kuwasaidiwa kwa namna mbalimbali ili wasijione wapweke.
Afisa Utumishi kutoka TSC, Judith Mtalai (kushoto) akikabidhi fedha kwa Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya Matumaini, Aurea Kyara kwaajili ya kuwakatia bima ya matibabu watoto wawili wa kituo hicho ambao hawakuwa na bima hiyo.

“Sisi ni wazazi, tuna watoto na tunalea, hivyo changamoto za watoto walio kwenye vituo kama hawa zinatugusa moja kwa moja. Ndiyo maana kwa umoja wetu tumekuja kuwaona na tumewaletea zawadi japo ni kidogo lakini tunaamini zitawasaidia,” amesema Mtalai wakati akiongea na watoto wa kituo cha Nyumba ya Matumaini. 

Akitoa neno la shukrani mara baada ya kupokea zawadi kwa niaba ya watoto, mwalimu na mlezi wa watoto wa kituo cha Cheshire Home, Getrude Nchudi alieleza kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini wanapopokea wageni wanaowasaidia watoto, nao pia wanapata moyo wa kuendelea kuwalea watoto.

“Tunasema asanteni sana kwa kujinyima kwenu, kutambua shida za watu wenye matatizo na kuweza kuwasaidia na kuwainua katika hali zao, karibuni tena maana mnatutia moyo, mnatuinua na kutupa nguvu za kuendelea kuwalea hawa watoto, Mungu awabariki na awazidishie pale mlipopunguza," amesema Mwalimu Nchudi.
Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya Matumaini, Aurea Kyara akiongea na watumishi wa TSC (hawapo pichani) wakati watumishi hao walipotembelea kituo hicho.

Naye Mkuu wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini, Aurea Kyara alieleza kuwa kwa sasa kituo hicho kinahudumia watoto 67 ambao wanaanzia umri wa miaka mitatu hadi miaka ishirini na tano na wanasoma madarasa tofauti kuanzia awali hadi ngazi ya chuo.

Aliweka bayana kuwa watoto wote wanagharamiwa na kituo hicho kwa kila kitu huku akieleza kuwa kwa sasa wanakabiliwa na upungufu wa fedha na wameshindwa kuwalipia karo ya shule wanafunzi waliokuwa wanawasomesha katika shule za binafsi.

“Tumewahamisha wanafunzi wengi wa shule ya msingi kutoka shule za binafsi na tumewasambaza kwenye shule za Serikali kwa kuwa hatuna fedha za kutosha kugharamia karo katika shule za binafsi,”amesema Kyara.
Picha ya pamoja kati ya watumishi wa Tume na mlezi wa kituo cha kulelea watoto cha Cheshire home, Mwl. Getrude Nchubi (Mtawa) wakati watumishi wa Tume walipotembelea kituo hicho na kutoa zawadi.

Aliwashukuru watumishi TSC kwa kuwatembelea huku akieleza kuwa wanakaribisha mtu yeyote anapenda kuwatembelea watoto hao na siyo lazima kuwa hadi awe na zawadi ndio aende kuwaona.

“Tunawashukuru sana kwa moyo wenu wa upendo, mnapokuja watoto hawa wanajisikia faraja na wanaona wamezungukwa na jamii ya watu wanaowapenda na kuwajali. Tunamkaribisha mtu yeyote anayependa kuja kuwaona na kuzungumza, sio lazima hadi awe na zawadi, kuja tu kuwaona ni jambo kubwa kwao,”amesema.
Picha ya pamoja kati ya watoto wa kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya matumaini na baadhi ya watumishi wa TSC waliotembelea watoto hao na kuwapa zawadi.

Kwa upande wa watoto hao, waliwashukuru watumishi wa Tume kwa kuwatembelea na kuomba watu wengine wenye moyo wa kuwajali wasisite kuwatembelea.

Watumishi wa TSC walikabibhi zawadi mbalimbali ikiwemo sabuni, matunda, vinywaji, mifagio, mpira wa kumwagilia bustani, fedha kwa ajili ya bima ya matibabu kwa watoto wawili wa kituo cha Matumaini pamoja na zawadi nyingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news