WANAHABARI WANAWAKE MKOANI MARA, DAWATI LA JINSIA WASAIDIA KITUO CHA WAZEE

NA FRESHA KINASA

Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wa Mkoa wa Mara (Visional Journalist Women) kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto mkoani humo wametoa msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali katika Kituo cha Kulelea Wazee wenye Ukoma kilichopo eneo la Nyabange Wilaya ya Butiama
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mara, Halima Kigera na Afisa Mwenzake kutoka dawati wakimkabidhi mfuko wa sabuni ya unga Afisa Mfawidhi Makazi ya Wazee na Walemavu Wasiojiweza Kituo cha Nyabange, Bena Mazaro mwenye ushungi kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Mara, Jovina Masano aliyebrba boksi la sabuni. 

Misaada hiyo ni pamoja na gunia moja la mahindi, Sabuni za miche za kufulia, sabuni za kuogea, sabuni za unga za kufulia, pamoja na mafuta ya kupaka na vinywaji (soda).

Misaada hiyo imetolewa leo Machi 10, 2021 kituoni hapo, lengo ni kuendelea kuadhimisha siku ya Wanawake duniani iliyofanyika Machi 8, mwaka huu kwa vitendo sambamba na kuonesha upendo na matendo ya huruma kwa vitendo kwa wahitaji.
Maafisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mara na Waandishi wa Habari Wanawake wakijiandaa kukabidhi misaada walipotembelea kituo cha kulelea Wazee wenye Ukoma Kilichopo Nyabange Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara. 

Mwenyekiti wa Kikundi Cha Waandishi wa Habari Wanawake (VJW) ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Jamhuri, Jovina Masano, amesema waliamua kuchangishana fedha wanakikundi pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kuwaunga mkono. Ambapo waliunganisha michango yao na Dawati la Jinsia Mkoa wa Mara kwenda kuwapatia wazee hao.

"Kikundi chetu Wanahabari Wanawake tuliona tuchangishane fedha sisi wenyewe, katika hili tuliwashirikisha baadhi ya wadau nashukuru walituunga mkono akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Caroline Muthapula. Tulitambua umuhimu wa Dawati la Jinsia na Watoto kwa kuwa wao wanashughulikia masuala ya ukatili tuliwashirikisha wakaafikiana na jambo hili, pia wakatoa michango yao na tumeweza kuitoa kwa pamoja iwasaidie wazee hawa,"amesema Jovina.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mara, Halima Miraji Kigera, amesema wazee wanapaswa kusaidiwa kutokana na kwamba, hawana uwezo wa kumudu kujihudumia wenyewe hivyo kuwakumbuka na kuwajali ni Jambo jema katika kuhakikisha wanapata mahitaji yao kama ilivyo kwa wengine.
Wazee wakiwa katika kituo kilichopo eneo la Nyabange Wilaya ya Butiama wakinywa (soda) ambazo ni miongoni mwa misaada iliyotolewa na Kikundi Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Mara wakishirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto Mkoani humo.

"Tumeshirikiana na wenzetu Waandishi wa Habari Wanawake kuwasaidia hawa wazee wetu, sote tunajua kwamba kwa sasa hawana nguvu ni jukumu la kila mmoja kuwajali na kuwapa mahitaji mbalimbali, enzi zao wakiwa na nguvu walitusaidia sisi kwa hiyo lazima turudishe fadhila hii haiishi tu katika kuadhimisha siku ya Wanawake bali tutaendelea kujitoa kuwakumbuka kadri Mungu atakavyotujalia,"amesema.

Aidha, Halima alitumia fursa hiyo, kuwaasa wazee hao kuishi kwa kumtegemea Mungu katika maisha yao yote pamoja na kupendana wao kwa wao wakati wote.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Mkazi ya Wazee na Walemavu Wasiojiweza katika Kituo hicho, Bena Mazaro akipokea misaada hiyo amepongeza hatua hiyo na kusema, kitendo hicho kilichofanywa ni cha kipekee na kinapaswa kuigwa na wengine kwani ni njia mojawapo ya kutekeleza amri ya upendo ulioagizwa na Mungu Kupitia vitabu vitakatifu.
Mwenyekiti wa Kikundi Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Mara (VJW), Jovina Masano akiteta Jambo na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kutoka Dawati la Jinsia Mkoa wa Mara Halima Kigera walipotembelea kituo cha kulelea Wazee wenye ukoma waliopo kituo cha Nyabange Wilaya ya Musoma kwa lengo la kutoa misaada yao. 

"Nawapongeza Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mara na Wanahabari Wanawake kwa kuungana kwenu pamoja kuja kuwasaidia Wazee hawa. Mmeonesha utu na kuwathamini sana wazee wetu, kitendo hiki kinawashinda watu wengi hata wenye kipato kikubwa. Mungu awazidishie mlipotoa na mzidi kufanya hivi tena hata wakati Mwingine,"amesema Bena.

Mwenyekiti wa wazee hao kituoni hapo George Ndege mbali na kushukuru, ameipongeza serikali ya Awamu ya Tano Chini ya Rais Dakt.John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuwahudumia kwa dhatiJambo ambalo linatija kubwa kwao.

"Tangu alipochaguliwa Rais Magufuli kuongoza Nchi yetu, naweza kusema tunaishi kwa amani, furaha na huduma mbalimbali kituoni hapa tunazipata yakiwemo mavazi kwa uhakika kwa niaba ya Wazee wote tunaoishi hao niseme kwamba Serikali inatujali japo Kuna changamoto kubwa moja ya umeme tunaiomba serikali isaidie kututua changamoto hii," amesema Mzee ndege.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news