Waziri Mkuu amuagiza RC mkoani Njombe kufuatilia madai ya wakulima wa chai

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie na kuchukua hatua kwa baadhi ya viwanda vya chai vinavyonunua majani mabichi ya chai ambavyo vimekuwa vikichelewesha malipo ya wakulima ahakikishe vinawalipa kwa wakati, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Njombe).

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Chai Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipoongoza Mkutano wao kwenye ukumbi wa Johnson, Njombe, Machi 10, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe minada ya kuuza zao la chai katika ukanda wa maeneo yanayozalisha zao hilo ili kuwarahishia wakulima kupata soko la uhakika na kuacha kutegemea minada ya nje ya nchi.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Machi 10, 2021 katika kikao na wadau wa zao la chai kilichofanyika katika ukumbi wa Johnson, mjini Njombe. Amesema Serikali itasimamia kikamilifu zao hilo na kuhakikisha wahusika wananufaika.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuona zao hilo linapata mafanikio, hivyo amewataka watendaji wafuatilie kuhakikisha wakulima wote wananufaika na zao hilo. ”Lazima wakulima walipwe fedha zao kwa wakati ili waweze kuhudumia mashamba yao na kukidhi mahitaji yao.”

Amesema zao la chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati hapa nchini na kwamba Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili liendelee kuwa na tija kwa wakulima, wenye viwanda na Taifa kwa ujumla.

“Zao la chai ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao hili huliingizia Taifa zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 60 kwa mwaka. Tukiboresha mikakati yetu litatuongezea fedha nyingi zaidi,"amesema.

Waziri Mkuu amesema zao la chai limechangia kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu zaidi ya 50,000 wameajiriwa viwandani na mashambani. Pia limetoa takribani ajira 2,000,000 zisizo za moja kwa moja. “Idadi hii haitoshi kulingana na ardhi nzuri tuliyonayo.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipoongoza Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Chai Tanzania kwenye ukumbi wa Johnson, Njombe, Machi 10, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji waje nchini kujenga viwanda vya kuchakata zao la chai kwa kuwa nchi ina mazingira mazuri ya uwekezaji na malighafi ya kutosha pamoja na nishati ya uhakika.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema suala la ucheleweshwaji wa malipo linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya chai halikubaliki, amewataka wawekezaji wote wawalipe wakulima fedha zao kwa wakati.

Kuhusu kuwepo kwa minada ya chai nchini, Waziri wa Kilimo amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es Salaam hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.

Naye, Mwenyekiti wa vikao vya wadau wa chai, Spika wa Bunge Mstaafu Anne Makinda ameiomba Serikali kuiwezesha Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) kwa kuipatia vitendea kazi na wataalamu ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe alimweleza Waziri Mkuu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa zao mkoani Njombe kuwa ni pamoja na baadhi ya viwanda vinavyonunua majani mabichi ya chai kushindwa kuwalipa wakulima fedha zao kwa wakati.

Zao la chai kwa hivi sasa linalimwa katika Wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro. Jumla ya eneo lililopandwa chai ni hekta 22,721 ambapo wakulima wakubwa wana hekta 11,272 na wakulima wadogo hekta 11,449.

Wastani wa asilimia 80 ya chai yote inayozalishwa nchini huuzwa kwenye masoko ya nje. Kati ya hizo wastani wa asilimia 40 huuzwa kupitia soko la mnada wa chai Mombasa na zilizobakia huuzwa moja kwa moja kwa wanunuzi katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Ujerumani, Pakistani, Falme za Kiarabu, Urusi na Marekani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news