Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Simon Anange pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhe. Joseph Kashushura Machi 3, 2021 wamepokea ujumbe kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, EPZA, TIC na Bodi ya Sukari ulioambatana na mwakilishi mkazi wa kampuni ya Mahashree Agroprocessing Tz Ltd mwenye nia ya kuwekeza kiwanda cha sukari na kilimo cha miwa, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Kasulu).
Baadhi ya wataalamu kutoka taasisi za serikali wakiwa na mwekezaji katika shamba lenye ukubwa wa hekta 37,662 lililotengwa maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na Halmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Viwanda na Biashara Mhandisi Ramson Mwilangali (wa kwanza kulia) akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Wilaya ya Kasulu na Mwekezaji aliyeonesha nia ya kuwekeza kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda.
Ziara hii imekuja mara baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John P. Magufuli aliyoitoa tarehe 12 Februari, 2021
alipokuwa akizindua kiwanda cha nafaka cha Mahashree Agroprocessing Tz
Ltd kilichopo Mkoani Morogoro.
Mhe. Rais aliiagiza Wizara ya
viwanda na Biashara kwa kushirikiana na EPZ na TIC kuhakikisha
wanampatia mwekezaji ambaye ni Mahashree Agroprocessing Tz Ltd eneo zuri
kwa ajili ya kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari ili
kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, kuleta ajira na kodi kwa serikali.
Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya Agroprocessing Tz Ltd ndugu Dhaval Maheshwari akifuatilia kwa makini kikao kati ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, wawakilishi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Eneo Huru la Uwekezaji (EPZA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kujadili uwekezaji wa eneo la kilimo cha mpunga na ujenzi wa kiwanda.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanali Simon Anange akizungumza wakati wa kikao na mwekezaji aliyeonesha nia ya kuwekeza kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha Sukari.
Katika kutekeleza agizo hilo la Rais, Wizara ya Viwanda na
Biashara kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekazaji (TIC) ilifanya jitihada
za upatikanaji wa shamba ambalo linapakana na mto Malagalasi lenye
ukubwa wa hekta 37,662. Shamba hili lipo katika kata tatu za Heru
Ushingo, Kitanga na Nyamidaho zenye vijiji saba ambavyo ni Nyarugusu,
Kiyungwe, Kitanga, Kumtundu, Nyamidaho, Kigadye na Heru Ushingo.
Baada
ya kuzungunguka na Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya Mahashree ndugu
Dhaval Maheshwari katika eneo la mradi ambalo lipo umbali wa kilometa 70
hadi 110 kutoka Makao makuu ya Wilaya ya Kasulu.
Baadhi ya wataalamu kutoka taasisi za serikali wakiangalia ramani ya shamba kumuonesha mwekezaji mwenye nia ya kuanzisha kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya Agroprocessing Tz Ltd ndugu Dhaval Maheshwari.
Mwakilishi
huyu wa mwekezaji alivutiwa zaidi na shamba hili ambapo amesema kuwa kwa
sasa watafanya upembuzi yakinifu ya ardhi na wakishakamilisha wataanza
na kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari ambapo kwa kiasi
kikubwa watahusisha wanakijiji wanaozunguka eneo la mradi kushiriki pia
katika kilimo cha miwa (Out Growers) kwa ajili ya malighafi ya kiwanda.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilzaya ya Kasulu Mhe. Kanali Simon Anange
amepogeza jitihada zinazofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara, TIC,
EPZA na Bodi ya Sukari (SBT) kwa kulichagua eneo la Kasulu kuwa kitovu
cha uwekezaji kwa kumleta mwekezaji ambaye ameonesha nia ya kuwekeza
katika kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amefanya
mazungumzo na mwakilishi wa mwekezaji na kumhakikishia ushirikiano wa
kila hatua ili kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa unaanza mapema kwani
Kigoma ni eneo zuri la uwekezaji hasa ukizingatia uwepo wa mto
malagalasi ambao unatiririsha maji ya kutosha na uwepo wa reli kwa ajili
ya usafirishaji wa mashine za kiwanda na bidhaa.