Wanajangwani wameendelea kuwatengenezea mazingira mazuri mahasimu wao Wekundu wa Msimbazi kuelekea kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuruhusu sare ya bao moja kwa moja, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Ni kupitia mtanange ambao Yanga SC imeucheza Machi 7, 2021 dhidi ya wenyeji Polisi Tanzania katika dimba la Sheikh Amri Abeid lililopo jijini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.
Sare hiyo imeifanya Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze kufikisha alama 50 baada ya kucheza mechi 23 ikiendelea kuongoza ligi kwa alama zaidi ya mabingwa watetezi, Simba.
Awali Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mrundi, Fiston Abdul Razak dakika ya 42 akimalizia kwa kisigino kazi ya winga Mkongo, Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia.
Hata hivyo, kiungo wa zamani wa Yanga, Pius Buswita aliyetokea benchi kipindi cha pili alileta majonzi kwa Wanajangwani baada ya kuisawazishia Polisi Tanzania dakika ya 90 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Deusdedit Cossmas ndani ya dimba hilo.
Katika mtanange huo, Polisi Tanzania ilimaliza pungufu baada ya beki wake, mkongwe Kelvin Yondani kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 87 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Sare hiyo inafanya Polisi Tanzania kufikisha alama 29 ma ipo nafasi ya nane huku Yanga SC ikiwa na alama 50 imecheza jumla ya mechi 23.
Kikosi cha Yanga kilikuwa na mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kurejea kwa nyota wao Ditram Nchimbi ambaye alikuwa anapambana na timu yake ya zamani ya Polisi Tanzania.
Awali Mshauri Mkuu wa masuala ya mabadiliko wa Yanga SC, Senzo Mbatha aliwaomba mashabiki wa timu hiyo waendelee kuwaunga mkono kwani uongozi unaendelea kupambana kuijenga timu hiyo ili izidi kuwa bora zaidi.
“Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, ulikuwa mchezo mgumu kutokana na ukweli kwamba wachezaji wetu walipambana, ili kupata matokeo mazuri lakini hali haikuwa kama ilivyokuwa matarajio yetu.
“Tunajua kuna vitu vingi ambavyo tunapaswa kuvirekebisha kama timu, na tuna imani benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Cedric Kaze tutaweza kumaliza mapungufu yaliyopo na kurejea tena katika hali ya ushindani kama ilivyokuwa awali,"alidai kabla ya mchezo huu.
Wakati huo huo Gwambina FC imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mabao ya Paul Nonga dakika ya 24 na Hamad Nassor dakika ya 71 yalipatikana katika dimba la CCM Gairo mkoani Morogoro.
Huku Coastal Union ikilazimishwa sare ya bila kufungana na KMC katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ikiwa ni mwendelezo wa mitanange ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tags
Michezo