Askofu Gadi amuomba Rais Samia kuwezesha uraia pacha kwa Watanzania Diaspora

Askofu wa Kanisa la Good News For All Ministry, Dk. Charles Gadi amemuomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kusaidia upatikanaji wa uraia pacha kwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini na kufanya kazi nje ya nchi.
Askofu wa Kanisa la Good News For All Ministry, Dk. Charles Gadi.

Ombi hilo amelitoa leo Aprili 21, 2021 jijini Dar es Salaam akati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema uraia pacha ni muhimu kwani utawawezesha raia waishio nje ya nchi (wanadiaspora) kuwa sehemu ya kuijenga nchi yao kwa kuwekeza mapato yao hapa nchini.

Amesema wakati wa serikali ya Awamu ya nne, Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete aliwashawishi watanzania waishio nje ya nchi kurudi kuja kuwekeza nchini.

Amesema wengi wao walirejea na kununua ardhi na majumba kadhaa, ikiwemo kuanzisha miradi ya kimkakati ya kimaendeleo lakini ghafla ndoto zao ziliimwa kutokana kuzuuliwa kutowekeza katika maeneo waliyoyachukua.

“Jambo hilo lilifanya baadhi yao kupotea mali zao, au kuhamisha majina na kuweka majina ya ndugu zao ili kuepuka kupoteza mali hizo, yakiwemo majumba, mashamba, ardhi na viwanja.

Askofu Gadi amesema raia waishio nje ya nchi wengi wao baada ya kufanya kazi huko kwa muda mrefu, wanatamani kurudi nchini kumalizia pensheni ya uzee wao hapa.

“Raia hawa wanarudi na ujuzi walioupata huko nje wa kuendesha biashara, kampuni, viwanda, pia wanakuja na uzoefu wao katika kulipa kodi maana huko nje hakuna mianya mingi ya ukwepaji kodi hivyo kwao swala la kodi ni swala la maisha ya kila raia.

“Hivyo kuwepo kwa uraia pacha kutawasaidia watu hawa kurudi nyumbani na kufanya kazi zao ambazo zitawezesha ukusanyaji wa mapato ya nchi kukua kupitia ulipaji wao wa kodi na uzoefu wao,” amesema

Aidha amesema watanzania hao wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi (diaspora) wanaweza kuwa msaada mkubwa katika uchumi wa nchi kwa kurejesha au kutuma fedha zao kwenye nchi yao kwa ajili ya uwekezaji na hivyo kuinua pato la taifa na kuzalisha ajira nyingi.

“Hali hiyo imezisaidia sana nchi za India, China, Kenya, Ethiopia, Nigeria na mataifa mengi ambayo yanafaidi sana uchumi utokanao na kitu kinachoitwa foreign remittance toka kwa wana diaspora (yaani raia wa nchi moja wanaoishi mataifa mbali mbali). Uchumi wa Kenya na Ethiopia ni mifano hai ya mafanikio hayo ya wanadiaspora,” amesema na kuongeza.

“Tunakuomba rais kama ulivyofanikiwa kurejesha matumaini makubwa kwa wawekezaji wa nje na ndani hasa sekta binafsi, vivyo hivyo urejeshe matumaini ya wanadiaspora wa kitanzania ili waweze kuurejesha uchumi wao hapa nchini na kulijenga Taifa letu,” amesema.

Aidha Askofu Gadi amemuomba Rais Samia kushughulikia swala la ardhi na umiliki wake ambapo amemuomba aanzishe mchakato wa kurekebisha sheria za ardhi ili wananchi na wawezekezaji wa ndani na nje waweze kuwa na uhakika wa umilikaji wa ardhi kwa lengo la kulinda mitaji yao na kuwa salama katika biashara.

“Kama sheria ya ardhi haziheshimiwi wananchi na wamilikaji wanakuwa kama watumwa kwenye nchi zao. Mfano Israeli waliwahi kuwa watumwa na Mungu akawasusia sherehe zao saba kwa sababu ya makosa ya wafalme wao kwenye swala la ardhi. Kwa hiyo kuacha kuheshimu sheria za ardhi au dhuluma yoyote kwenye ardhi ni kuwafanya wananchi au taifa husika kuwa kama watumwa milele,” amesema

Hata hivyo amesema suala la uboreshaji wa mipango miji, kwa kuweka utaratibu wa kuondoa mashamba yaliyoko kati kati au karibu na miji si jambo zuri.

Amesema mashamba hayo husaidia kurekebisha hali ya hewa na kuondoa hewa ya ukaa kwenye miji, na hata baadhi ya wanyama wa kufungwa kupata malisho au chakula chake humo.

Aidha amesema kuwa anampongeza kwa dhati Rais Samia kwa kupata heshima ya kuiongoza nchi ya Tanzania katika awamu hii ya sita.

“Tunamshukuru Mungu kwa jitihada za dhati alizochukua tangu apokee kijiti toka kwa mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli, za kurejesha matumaini mapya kwa watanzania katika sekta za biashara, sekta binafsi na nyingine mbali mbali katika taifa letu.

“Tutaendelea kumwombea kwa Mungu kwa dhati ili aweze kufanikiwa katika nia yake njema ya kulijenga taifa letu kiuchumi, amani na umoja, kiafya, kielimu na kiutamaduni,” amesema Askofu Gadi. (2eyezmedia).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news