
"Makamu, tunakuomba sana suala hili mulione na mulizungumze, Ikibidi hata kama ni mgao unaotolewa kuhusu mazingira, basi utufike na utufike kwa wakati, Kwani hata huku Zanzibar wapo watu wenye weledi katika suala la kimazingira, lakini kama kuna changamoto, basi ndio eneo sahihi kwetu kuweza kujifunza,"amesema Mwenyekiti huyo wa kamati na ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Welezo.
Mheshimiwa Hassan alielezea jinsi ambavyo kuingizwa suala la mazingira katika Muungano kunavyoikosesha Zanzibar fursa, misaada na miradi ya moja kwa moja, kwa kuwa shughuli zote zinazohusiana na suala hilo humalizika Tanzania Bara, na inapotokea kuletwa Zanzibar huwa ni kwa hatua za utekelezwaji tu.
Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud, aliwaambia wajumbe hao waliokwenda kumtembelea ofisini kwake kwa ushauri kwamba ni kweli kuwa suala la mazingira ni sehemu ya Muungano kwa muda mrefu sana, ila akasema kuwa, "Ni wakati sasa kuzungumzwa na kuweza kusawazishwa ili kila upande wa Muungano uweze kunufaika.”
"Kwa sasa inabidi tumtumie sana waziri wetu, Mheshimiwa Saada Mkuya, ili kututafutia wafadhili binafsi kutoka maeneo mbali mbali ya dunia ili nasi Zanzibar tuweze kunufaika moja kwa moja na miradi ya mazingira,” amesema Makamu huyo wa Rais, huku akiitaka kamati hiyo kuendelea kuwa karibu na ofisi yake ili iwe na msaada zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande mwingine, Kamati hiyo kupitia mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hassan, iliomba msaada zaidi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika kuzipa msukumo Tume ya Ukimwi Zanibar na Idara ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Zanzibar ili kuweza kupunguza na kuondoa kabisa matatizo hayo.
”Ukimwi na madawa ya kulevya yamekuwa yakipoteza sana nguvu kazi ya vijana wa taifa hili,” amesema Makamu wa Kwanza wa Rais akiongeza kwamba Ofisi yake inayachukulia masuala yote hayo kwa umuhimu mkubwa na kwamba muda wowote ipo tayari kutoa muongozo na usimamizi, isipokuwa akazidi kusisitiza mashirikiano na mshikamano.
Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi ilikutana na Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mashauriano na mazungumzo ya kikazi.