Bodi ya Wakurungezi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imetoa wito kwa halmashauri kutumia tafiti na teknolojia za kilimo bora zinazobuniwa na watafiti wa taasisi hiyo ili kuwasaidia wakulima kujikita katika kilimo bora na cha kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Yohana Budeba alitoa wito huo wakati wa ziara ya Bodi hiyo ya kutembelea na kujionea kazi zinazofanya na Kituo cha Utafiti cha Naliendele (TARI Naliendele) mkoani Mtwara.
“Halmashauri zihimizwe kuunga juhudi zinazofanywa na Taasisi yetu ya utafiti ambayo inafanya kazi kubwa na nzuri katika kutafiti na kubuni teknolojia za kubadilisha kilimo chetu kuwa bora,” amesema Budeba.
Aidha, Budeba amesema kuwa utafiti ni gharama kubwa na serikali imekuwa ikigharamia tafiti mbalimbali kupitia taasisi hiyo ili kuboresha na kuendeleza kilimo cha kisasa kwa manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla.
Tags
Habari