Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimefanya uchaguzi wa Rais ambapo Dkt. Edward Hoseah ameibuka mshindi wa nafasi hiyo kwa kupata kura 297 katika uchaguzi uliojaa ushindani mkali, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Arusha).
Dkt. Edward Hoseah ambaye ni Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Aprili 16, 2021 jijini Arusha, mshindani wa karibu wa Dkt. Hoseah Flaviana Charles amepata kura 223.
Dk. Hoseah amewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt.John Magufuli kutengua uteuzi wake mwaka 2015.
Kwa ushindi huo Dk. Edward Hoseah sasa anachukua nafasi ya Rais wa TLS anayemaliza muda wake Dk. Rugemeleza Nshala ambaye naye alichukua kijiti cha kuiongoza TLS kutoka kwa mtangulizi wake Fatma Karume.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi Charles Rwechungura amemtangaza Dkt. Hosea kuwa mshindi kwa kura 297 na kuwashinda wenzake wanne aliokuwa akichuana nao katika kiti nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi katika chama hicho kinachosimamia misingi ya haki na sheria.
"Dkt. Edward Hosea amepata kura 297, kwahiyo naona hamukushangilia sana kwasababu mmeshajua haya mambo, tumepata fununu kuna mtu alitusaliti lakini sisi tumesema tulichonacho ndio hicho," alisema Rwechungura alipokuwa anamtangaza Dkt Hosea kuwa rais wa TLS
Tags
Habari