Dunia bila Malaria inawezekana- Guterres

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria duniain ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia ujumbe wake kupongeza nchi ambazo zimefikia lengo kubwa la kutokomeza ugonjwa huo hatari akisema zimeonesha "kwa pamoja dunia isiyo na Malaria inawezekana."

Guterres amesema licha ya janga la Corona au COVID-19, idadi ya nhi zinazokaribia kufikia lengo la kutokomeza Malaria inaongezeka.

"Katika nchi ambako Malaria haiko tena, watu wote, bila kujali uraia au utaifa wao , na bila kujali wana uwezo wa kulipa au la, wamefikiwa na huduma wanazohitaji ili kuzuia, kubaini au kutibu Malaria. Ufadhili endelevu katika huduma za Malaria na mifumo thabiti ya ufuatiliaji na ushiriki wa jamii ndio siri ya mafanikio," amesema Katibu Mkuu.
Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya. (Sven Torfinn/WHO 2016).
 
Hata hivyo amesema, wakati dunia inasherehekea mafanikio hayo, "hebu tusisahau kuwa mamilioni ya watu duniani kote, wanaendelea kuugua au kufariki dunia kutokana na Malaria. Kila mwaka Malaria husababisha vifo vya watu zaidi ya 400,000, wengi wao ni watoto wadogo barani Afrika. Na kila mwaka, kuna zaidi ya wagonjwa wapya milioni 200 wa Malaria."

Guterres amesema Malaria inaweza kutokomezwa kwa utashi thabiti wa kisiasa, uwekezaji wa kutosha na mikakati mchanganyiko.

Kutokomeza Malaria

Kati yam waka 2000 na 2019, idadi ya nchi zenye wagonjwa wapya wa Malaria chini ya 100 ziliongezeka kutoka 6 hadi 27.

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, linasema kiwango hicho ni kiashiria thabiti kuwa hatua ya kutokomeza Malaria inaweza kufikiwa na kupongeza nchi ambazo zimeshafikia lengo hilo.

WHO inasema nchi hizo zinatoa hamasa kwa mataifa mengine yanayojitahidi kuondokana na ugonjwa huo na kuimarisha afya na njia za kujipatia kipato kwa wananchi wao.

Uchambuzi kimataifa
Maendeleo katika kudhibiti malaria yalikuwa miongoni mwa sababu eneo la Afrika la WHO lilipata ongezeko kubwa zaidi la umri wa kuishi tangu 2000 kwa miaka 9.4 hadi miaka 60. (UNICEF / Adenike Ademuyiwa).
 
Mwaka 2019, bara la Afrika lilibeba mzigo wa asilimia 94 ya wagonjwa wote wa Malaria na vifo vitokanavyo na Malaria duniani, ambapo kati ya visa hivyo, zaidi ya nusu ni katika mataifa matano tu.

Nigeria asilimia 27, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, asilimia 12; Uganda na Niger asilimia 5 kila moja na Msumbiji asilimia 4.

Wakati wa kipindi hicho hicho, takribani asilimia 3 ya wagonjwa wa Malaria waliripotiwa nchi za kusini-mashariki mwa Asia na asilimia 2 katika ukanda wa Mediteranea Mashariki.

Ukanda wa Amerika na Pasifiki ulikuwa na wagonjwa wachache sana wa Malaria kama asilimia moja tu ya visa vyote duniani.

Kuthibitisha kutokuwepo na Malaria

Uthibitisho wa kutokomezwa kwa Malaria, ni kutambuliwa rasmi na WHO kuwa eneo fulani halina kabisa Malaria.

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa linatoa cheti hicho pindi nchi inapokuwa imethibitisha pasi shaka, kuwa mnyororo wa maambukizi ya Malaria umesambaratishwa nchi nzima kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Kufuatia miaka 50 ya juhudi za serikali na wanachi wa El Salvador za kutokomeza Malaria, mwezi Februari mwaka huu, taifa hilo la America ya Kati lilikuwa taifa la kwanza kwenye ukanda huo kuthibitishwa na WHO kuwa halina tena Malaria.

Wakati huo huo, China nayo haijawa na mgonjwa wa Malaria tangu mwaka 2016 hadi leo na mwaka jana wa 2020 taifa hilo liliwasilisha ombi lake WHO ili lithibitishwa kuwa halina tena Malaria. (UNnews).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news