Hotuba fupi ya Rais Samia yawafuta machozi wafanyabiashara nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kwenda kuongeza idadi ya walipa kodi na kutotumia nguvu nyingi katika ukusanyaji wa mapato, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).

Wito huo ameutoa leo Aprili 1, 2021 baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana wakiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri na Manaibu Waziri katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Rais Samia amesema kuwa,wanapaswa kwenda kutanua wigo wa walipa kodi nchini na kuhakikisha wanatumia akili katika ukusanyaji mapato kuliko kutumia nguvu.

''Naomba mkaongeze walipa kodi, hii trend mnayoenda nayo si nzuri, mnatumia nguvu sana kuliko akili katika kukusanya mapato, mnaowachukulia vifaa vyao na kufunga akaunti wakitoka hapo wanaenda kufunga biashara wanahamia nchi ya pili,''amesema.

Pia Rais Samia amewapongeza mawaziri kwa kuendelea kuwepo katika kusaidia majukumu mbalimbali na kuwataka wakafanye kazi kwa pamoja ikiwa wapo kwenye bunge la bajeti kwani bila bajeti ya serikali hakutokuwa na fedha.

''Niwapongeze mawaziri wote kwa kuendelea kuwepo kwenye kusukuma jahazi letu. Niwaambiwe jahazi hili upepo uzidi au uwe mdogo ni lazima liende,''amesema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango atoa agizo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba kuanza kushughulikia utatuzi wa masuala ya kifedha katika pande mbili za muungano.
 
Dkt.Mpango amesema, agizo hilo alipewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu na kwa vile mrithi wa Wizara ya Fedha na Mipango ameshapatikana ataanza na kazi hiyo pamoja na Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo.

"Jana nilikaa nikitafakari agizo lako hasa huyu mchawi ambaye amekuwa anashindwa kutatau masuala ya mahusiano ya kifedha katika pande zote mbili za muungano sasa nimepewa huyo mtoto nimepewa huyo mtoto nifanye hiyo kazi, sasa nimepata mrithi Mhe. Rais nakushukuru sasa nimepata mrithi Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba hii ndo iwe kazi kazi yako ya kwanza," amesema Dkt. Philip Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango ameahidi kufuatilia kwa ukaribu juu ya mvutano uliopo baina ya mawaziri na manaibu waziri, na kuwaagiza mawaziri kuwapatia kazi za kufanya manaibu waziri huku akimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kwenda kushughulikia tatizo kama hilo kwa makatibu wakuu na manaibu katibu wao.

"Mhe. Rais ulikemea kwa nguvu utaratibu wa mawaziri na naibu waziri kuvutana vutana natumaini walisikia na hili tutalifuiatilia, tunajenga nyumba moja hakuna sababu ya kuvutana," amesema Dkt. Philip Mpango.Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini katika Serikali yake na kumuahidi kuendelea kuitumikia nafasi hiyo akifuata maelekezo yake kwa weledi mkubwa.

Amesema, ni jambo la kumshukuru Rais kwa kumuamini katika nafasi hiyo ya uwaziri mkuu licha ya jana kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza la mawaziri.

Waziri Mkuu Majaliwa ametumia nafasi hiyo kumpongeza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Katanga akimsifu kwa namna ambavyo amekua akifanya kazi kwa uaminifu na mafanikio kwenye nafasi zote alizowahi kuzishika.

"Nimpongeze sana Balozi Katanga namfahamu vizuri sana amekua Katibu Mkuu wangu nikiwa TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), nimhakikishie ushirikiano na kwa mawaziri wenzangu tunaahidi kwako Rais kuwa tupo tayari kuwatumikia watanzania. Tukuahidi kwamba tutaendelea kukupa heshima na kutunza uaminifu wako kwetu tukifanya kazi kwa weledi, lengo likiwa kutekeleza ahadi za serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwatumikia wananchi kwa asilimia 100,"amesema Majaliwa.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Yahaya Katanga amesema, Rais Samia ameonyesha imani kubwa kwake kwa kumteua hivyo atafanya kazi kwa maelekezo yake na kwa mujibu wa kiapo.

Balozi Katanga amesema leo ndio siku ambayo alitakiwa kurudi katika kituo chake cha kazi cha Ubalozi wa Tanzania nchini Japan, lakini imembidi kuihairisha safari hiyo ili kuendelea na majukumu makubwa aliyokabidhiwa kwa sasa hapa nchini.

Pia amesema kazi kubwa ya kufanya ni kuhakikisha serikali inakuwa makini katika kuendesha safari iliyoanza ya kufikia mwaka 2025 katika kuharakisha maendeleo hapa nchini.

"Jana nilishangaa nachukuliwa tu napelekwa huku na huko hadi uwanja wa ndege nikaambiwa nitulie hapa, natakiwa kwenda Dodoma hayo mengine nitayajua huko huko, basi nikiwa pale uwanja wa ndege ndio nikaona hotuba yako kwenye televisheni ukiniteua, nashukuru sana.Leo nilikuwa nirudi Japan kwa maelekezo ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na tiketi ile ya Japan ikabidi niahirishe,"amesema Balozi Katanga.

Balozi Katanga amesema, atafanya kazi kwa bidii huku akiahidi ushirikiano na uzalendo katika majukumu hayo mapya ili kuyafikia matokeo chanya mapema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kuwa Waziri wa Fedha na Mipango katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 01 Aprili 2021. (Picha na Ikulu).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news