Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imefanya ziara katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Mikumi kukagua maendeleo ya kazi inayoendelea kufanywa na kikosi kazi cha operesheni umeme kwenye Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP-MW2115) mkoani Morogoro, anaripoti John Bera (WMU).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Wa kwanza kulia) akiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Viongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) wakikagua maeneo mbalimbali ya ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la (JNHPP-MW2115) wakati wa ziara ya viongozi hao ya kukagua eneo ambalo miti yake inatakiwa kung’olewa ili kupisha ujenzi wa Bwawa la maji kwa ajili ya kufua Umeme.
Kamati hiyo imeridhishwa na na kazi ya usafishaji wa eneo la mradi huo ambapo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema Wizara ya Maliasili na Utalii katika mradi huo ni mlengwa kwa kuwa eneo ambalo mradi unatekelezwa ni hifadhi.
"Tumetoa eneo kubwa ambalo lilikuwa Hifadhi ya Nyerere, sisi ni wadau wakubwa wa eneo hili,"amefafanua Naibu Waziri Masanja.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja, Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na baadhi ya viongozi wa Taasisi za Uhifadhi za Wizara ya Maliasili na Utalii wakiangalia kazi inayoendelea ya ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua Hifadhi ya Taifa ya Nyerere pamoja kuangalia zoezi la ung’oaji wa miti katika eneo hilo.
Amesema, pamoja na kutoa eneo hilo bado wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa shughuli za kusafisha maeneo yote ya mradi huo.
"Tumefika katika kambi hii ambayo inasimamiwa na jeshi wamesafisha eneo kubwa na kwa asilimia 57 wameshatekeleza imebaki kama asilimia 43,kamati imekuja kuangalia utekelezaji na hasa usafishaji wa eneo hili ambapo miti inayokatwa inachakatwa ili kupatikana mbao na kuuzwa kwa wadau mbalimbali na fedha kuingizwa kwenye mfuko wa Serikali,"amesema Naibu Waziri.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi ya Maliasi na Utalii, Dkt. Aloyce Kwezi (wapili kulia) akielezea umuhimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaweka vivutio vya Utalii vitakavyo zunguka eneo la Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere pindi litakapokamilika ili kuvutia wageni wengi zaidi wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere mkoani Morogoro. Wa pili Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja, Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo ( wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine walioshiriki katika ziara hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Aloyce Kwezi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo amepongeza kazi kubwa inayoendelea kufanyika katika eneo hilo huku akiuelezea mradi huo kuwa sehemu ya utalii, hivyo Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuandaa miundombinu mizuri kwa ajili ya utalii.
""Nawapongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya pia watumishi wa TANAPA,TAWA na TFS na wizara nzima, tumeridhishwa na maendeleo ya zoezi hili kupitia operesheni umeme ambalo limefikia asilimia 57,"amesema Dkt.Kwezi.
Ametoa wito kwa wizara zinazohusika na mradi huo kushirikiana kwa pamoja ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.
Tags
Habari