Ligi Kuu Tanzania Bara yazidi kuwa ngumu, Yanga SC yaondoka na ushindi mwepesi kwa Biashara United

Klabu ya Yanga imefanikiwa kujikusanyia alama tatu zote baada ya kuibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya vijana wa Biashara United kutoka mkoani Mara, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Temeke).

Mtanange huo wa Aprili 17, 2021 ambao ulikuwa mkali ulizikutanisha timu hizo katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Yacouba Sogne ndani ya dakika ya 58 akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto, Adeyoum Saleh ndiye aliyewanyanyua mashabiki wa Yanga SC.

Kutokana na matokeo hayo, Wanajangwani wanaendelea kusalia katika kilele cha Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania kwa alama 54 baada ya kuzipiga mechi 24.

Wakati huo huo, wanalambalamba wa Azam FC wanaendelea kusalia nafasi ya pili kwa alama 50 baada ya kucheza michezo 25.

Nafasi ya tatu katika Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inashikiliwa na Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kwa alama 49.

Aidha, wanatarajiwa kucheza na Mwadui FC mjini Shinyanga ambapo tayari wamecheza mechi 21 katika msimamo huo.
 
Tayari nyota 28 wa kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu ya Simba wapo Nyanda ya Ziwa kwa ajili ya michezo mitatu ya Ligi ukiwamo mtanange dhidi ya Mwadui utakaopigwa leo.

Simba ambayo ilikuwa kwenye majukumu ya kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ilirejea wiki iliyopita na kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar na kushinda bao 5-0.

Kwa mujibu wa tovuti ya Simba imeandika kuwa Kocha Didier Gomez na wasaidizi wake, wameamua kuondoka na kikosi kizima kutokana ugumu wa mechi huku timu zote zikiwa zimejipanga kipindi hiki cha lala salama ligi ikielekea ukingoni.

Ratiba ya michezo hiyo Kanda ya Ziwa itaanza leo Jumapili ambapo itashuka kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga kuikabili Mwadui na siku tatu baadaye yaani Jumatano itacheza na Kagera Sugar Kaitaba kabla ya kumalizana na Gwambina Aprili 24.

Kikosi Kamili kitakachokwenda Kanda ya Ziwa;

Makipa:- Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim

Mabeki:-Shomari Kapombe, Joash Onyango, Pascal Wawa, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, David Kameta

Viungo:Jonas Mkude, Rally Bwalya, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Bernard Morrsion, Francis Kahata, Taddeo Lwanga.

Washambuliaji:Medie Kagere, John Bocco, Ibrahim Ajib, Kope Mugalu, Miraji Athumani, Perfect Chikwende.

Mbali na hayo, Coastal Union wamewachapa Ruvu Shooting 2-1 katika mchezo wa wao uliochezwa katika dimba la wa Mkwakwani,Tanga.

Rashid Chambo ndani ya dakika ya 42 na Ayoub Masoud dakika ya 63 ndiyo walifanikisha mabao hayo huku Ruvu Shooting likipashikwa na Fully Zullu Maganga dakika ya 21.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news