Mameneja Biashara wa Mamlaka za Maji Nchini wamesisitizwa kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji wa mapato ili kuboresha na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wa maeneo yao ya huduma, anaripoti Mohamed Saif (Mwanza).
Wito huo umetolewa Aprili 7, 2021 jijini Mwanza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ufunguzi wa mkutano uliokutanisha Mameneja Biashara wa Mamlaka zote za Maji nchini.
Mwenyekiti wa Mameneja Biashara wa Mamlaka za Maji Tanzania ambaye ni Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Tabora (TUWASA), Biswalo Benard akizungumza wakati wa mkutano.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele akifungua rasmi kikao cha Mameneja Biashara wa Mamlaka za Maji Tanzania kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.
“Suala la mauzo na mapato yaani makusanyo kwa ujumla tunawategemea nyinyi, ni muhimu mkatambua bila makusanyo mazuri Malaka za Maji hazitoweza kujiendesha,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele alisema changamoto miongoni mwa mamlaka za maji nyingi zinafanana ikiwemo ya uwepo wa wadaiwa sugu na upotevu wa maji na hivyo aliwasisitiza kutumia mkutano huo kuzijadili kwa kina na kuweka njia bora ya kukabiliana nazo kwa lengo zima la kuhakikisha huduma ya maji inaimarika.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria mkutano wa Mameneja Biashara wa Mamlaka za Maji Tanzania.
Meneja Biashara wa MWAUWASA, Meck Manyama akizungumza wakati wa mkutano wa Mameneja Biashara wa Mamlaka za Maji Tanzania.
“Mtakachojadili na kujifunza hapa mkichukulie kwa umuhimu wake na mtakaporudi kwenye taasisi zenu mhakikishe mnazifanyia kazi ili kupatikane tija iliyokusudiwa,” alielekeza Mhandisi Msenyele.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walipata fursa ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo na umuhimu wa mkutano husika katika kuzijadili kwa upana wake sambamba na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kukabiliana nazo.
Meck Manyama, Meneja Biashara kutoka MWAUWASA alisema kikwazo kikubwa wanachokabiliana nacho katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ni uwepo wa wadaiwa sugu waliositishiwa huduma ya maji muda mrefu lakini hawajajitokeza kulipa madeni yao.
“Hawa wadaiwa sugu wanatukwamisha kuboresha huduma, sisi hatuna ruzuku tunajiendesha kwa fedha zitokanazo na malipo ya ankara za maji ili kulipia umeme, kununua madawa na kukarabati miundombinu sasa inavyotokea baadhi ya wateja kushindwa kulipa inatuwia ngumu kuboresha huduma,” alifafanua Manyama.
Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Dodoma (DUWASA), Alex Mpagama akizngumza na waandishi wa habari.
Naye Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Dodoma (DUWASA), Alex Mpagama alibainisha kwamba mamlaka inadai wateja wake zaidi ya shilingi bilioni 1.7 fedha ambayo ilipaswa kutumika kuboresha huduma kwa wakazi wa Dodoma.
Hata hivyo alibainisha kwamba tayari baadhi ya wateja wameanza kupunguza madeni yao kwa kulipia madeni yao kwa awamu na alisisitiza wengine ambao bado kujitahidi kufanya ili kuipa nguvu DUWASA ya kuboresha hali ya upatiknaji wa huduma ya maji.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa ujumla wake, Mwenyekiti wa Mameneja Biashara ambaye ni Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Tabora (TUWASA), Biswalo Benard alisema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto zinazowakabili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kupambana nazo.
Tags
Habari