Klabu ya Manchester United imepiga hatua kubwa kuelekea nusu fainali ya Ligi ya Europa kutokana na ushindi wa ugenini dhidi ya Granada katika mchezo wa kwanza wa mechi yao ya mwisho ya nane, anaripo Mwandishi DIRAMAKINI.
Picha na beinsports
Mabao ya Marcus Rashford dakika ya 31 na Bruno Fernandes dakika ya 90 usiku yameipa Manchester United ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Granada.
Ni katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali UEFA Europa League Uwanja wa Nuevo Los Cármenes mjini Granada.
Aidha, timu hizo zitarudiana Aprili 15, mwaka huu katika dimba la Old Trafford na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya Ajax na AS Roma ambapo awali Roma imewafunga Ajax 2-1 mjini Amsterdam.
Hayo yanajiri ikiwa pia kikosi cha kocha Mikel Arteta cha Arsenal kilitoshana nguvu baada ya kutoa sare ya goli 1-1 dhidi ya Slavia Prague katika mchezo wa Ligi ya Europa robo fainali mkondo wa kwanza.
Ingizo jipya kutokea bechi Nicolas Pepe aliipatia timu yake ya Arsenal bao dakika ya 86, lakini bao hilo lilisawazishwa dakika ya mwisho ya mchezo.
Tomas Holes alifunga goli hilo kwa Prague akifanya mchezo wa raundi ya kwanza kumalizika kwa sare ya bao 1-1.