Angelina Masumbuko (17) mkazi wa mkazi wa Kijiji cha Nyasarwa Kata ya Bugulula Wilaya ya Geita, ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa tuhuma ya kosa la kuiba mtoto mchanga mwenye umri wa siku kumi na nne ili aweze kunusuru ndoa yake, anaripoti Robert Kalokola (DIRAMAKINI) Geita.
Tukio hilo lilitokea Machi 12, mwaka huu saa mbili na nusu usiku baada ya mtuhumiwa kuchukua mtoto wa Juliana Milichades bila taarifa na kutolea naye maeneo yasiyo julikana bila kuwajulisha wazazi wa mtoto.
Kamanda wa Polisi wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandamizi Henry Mwaibambe. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini ).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi linamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi.
Henry Mwaibambe amesema kuwa, mtuhumiwa baada ya mahojiano na jeshi la Polisi alieleza kuwa sababu ya kuiba mtoto huyo ilikuwa amdanganye mume wake ili ndoa yake isiyumbe kwasababu anataka mtoto na hajabahatika kupata.
Kamanda Mwaibambe amesema, kabla ya kutenda kosa hilo taarifa zinaonyesha mtuhumiwa baada ya mwenzake kujifungua aliweka mazoea ya ghafla kwenda kumtembelea na kumsaidia shughuli za ndani ingawa hawakuwa wakifahamiana vizuri na mazoea ya aina hiyo hayakuwepo.
"Siku moja mama wa mtoto akiwa nje amemlaza mtoto ndani, alikuja hakumukuta mtoto, majirani kwa kushirikiana na huyu mama walimtilia wasiwasi mama ambaye alikuwa anakuja kusaidia kazi, kwani yeye ndio alikuwa ameleta mazoea kwa mtoto kwa hiyo aprili 22 mwaka huu akakamtwa akiwa na huyo mtoto.
"Huyo mtoto tulimpeleka hospitali, tukampima na akaonekana ana afya njema ikabidi huyu mtoto tumkabidhi kwa mama yake, tukamhoji mtuhumiwa kwa nini umefanya kitendo hiki cha kuiba mtoto, akadai yeye ndoa yeke inayumba, mme anahitaji mtoto kila wakati, hivyo alifanya kumuridhisha mme wake," alieleza Mwaibambe.
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi linamshikilia Stephano Gerald (32) kwa kosa la kusababisha kifo cha mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Vitus Gerald mwenye umri wa miaka nane.
Tukio hilo la kifo linaelezwa kutokea usiku wa kuamkia tarehe 28 aprili Mwaka huu saa tatu na nusu usiku wakati Gerald Stephano akiwa amelewa anapigana na mke wake walimuangukia mtoto huyo na kufariki kwa kukosa Hewa.
"Wakiwa wanapigana na mke wake, waliangushana na kwenda kumlalia huyu mtoto, ambaye alikuwa amelala usingizi na mtoto akakosa hewa akafariki na mama wa mtoto kutokana na ugomvi huo amelazwa kituo cha afya bwanga na hali yake inaendelea vizuri," alisema Mwaibambe.
Kamanda ameongeza kuwa sababu za wanandoa hao kupigana zinaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi na kwamba mtoto huyo alikuwa hasomi shule.
Aidha, Jeshi la Polisi linachunguza kifo cha Beatrice Sylvanus (29) ambaye ni mfanyabiashara wa Duka aliyekutwa ameuawa barabarani tarehe 28 majira ya saa nne usiku muda mfupi baada ya kushushwa kwenye pikipiki (bodaboda) iliyompeleka nyumbani kwake akiwa na mtoto wake mgongoni.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe ameeleza kuwa uchunguzi umebaini marehemu alipigwa na kitu kizito kichwani na eneo hilo liko karibu na msitu.
Mwaibambe amefafanua kuwa Jeshi la polisi linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Fikiri Ezekiel ambaye ni Dereva wa Bajaj mkazi wa Mwabasabi wilayani Geita mkoani hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe watuhumiwa wote watafikishwa Mahakamani baada ya Upelelezi kukamilika ili haki iweze kutendeka
Kwa nyakati tofauti wakazi wa Geita wameieleza DIRAMAKINI kuwa, tukio hilo ni la kushangaza na wazazi hawapaswi kumuamini kila mtu.
Tags
Habari