Mbunge mstaafu Hamoud Jumaa aibuka kidedea Mjumbe Mkutano Mkuu Taifa

Mbunge mstaafu wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa (CCM) ameibuka kidedea kwa kushinda nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu Taifa katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi hiyo uliofanyika juzi katika ukumbi wa ofisi ya CCM uliopo Mlandizi Kibaha, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Kibaha).
Mbunge mstaafu wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa (CCM).

Jumaa ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 61 kati ya kura 74 za wajumbe wote licha ya kuwa siku ya uchaguzi hakuwepo ukumbini kwa kuwa alipata safari ya dharura na hivyo kuombewa kura na mmoja wa viongozi wa chama.

Uchaguzi wa nafasi hiyo muhimu katika chama umesimamiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Martine Ntemo,Katibu wa CCM Kibaha Vijijini, Rukia Mbasha na Mwenyekiti wa chama, Ludovick Lemmy.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Pwani, Kulwa Daudi amemtaja Jumaa kuwa mshindi halali wa nafasi hiyo.

Daudi amesema kuwa, Jumaa alipata kura 61 dhidi ya Rajabu Mtoi aliyepata kura 8 ,Mary Muya(4),Maria Sengerema (1),huku Tina Makanzu na Zuhura Seseme wakipata (0) huku kura zilizopigwa ni 74.

Aidha,Daudi alisema kuwa kufanyika kwa uchaguzi huo kulitokana na nafasi hiyo kuachwa wazi na mbunge wa sasa wa jimbo hilo Michael Mwakamo na kwamba uchaguzi huo umefanyika kwa muongozo na utaratibu uliowekwa na chama.

"Ndugu wajumbe kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Hamoud Jumaa kuwa ni mshindi wetu wa nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kwakuwa ndiye mgombea aliyepata kura nyingi zaidi ya wenzake wote,"amesema Daudi.

Nae Diwani wa Kata ya Mtambani, Godfrey Mwafulilwa (CCM) alisema kuwa, Jumaa ni mwanachama wa CCM ambaye amekuwa mtiifu na mzalendo kwani kitendo cha kurudi kugombea nafasi hiyo katika chama kimeonyesha ukomavu wa kisiasa.

Mwafulilwa alisema kuwa, Jumaa amekuwa mbunge wa Kibaha Vijijini kwa vipindi viwili lakini licha ya kukosa ubunge bado ameona arudi kuungana na wanachama wenzake ili kusaidiana katika kukiimarisha chama chake.

Alisema kuwa,angekuwa mtu mwingine ni wazi kuwa angekisusa chama na wala tusingemuona na kwamba kitendo cha kurudi katika chama ni uzalendo na anapaswa kuigwa na wengine.

"Binafsi nimeshangaa kuona Jumaa anashinda wakati hayupo ukumbini,kilichofanyika ni mmoja wa viongozi kumuombea kura lakini wajumbe wamempa kura na hatimaye Jumaa kushinda tena kwa kura nyingi ,"alisema Mwafulilwa.

Jumaa mara baada ya uchaguzi amesema kuwa, kukosa ubunge sio sababu ya kukitenga chama na kwamba ataendelea kuwa mwanachama wa CCM muda wote wa maisha yake.

Jumaa amesema kuwa, uongozi ni kubadilishana vijiti na hakuna sababu ya kugombana wala kufanya siasa za chuki kwakuwa wote wanajenga chama kimoja na ukiona mtu analeta chuki kwa mwenzake ni wazi kuwa sio mkomavu wa kisiasa.

"Mimi nilichukua fomu ya kugombea nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa lakini siku ya uchaguzi sikuweza kubahatika kushiriki kwakuwa nilipata safari ya dharura lakini niliombewa kura na wajumbe walinipigia,"amesema Jumaa

Hata hivyo,Jumaa amesema kuwa,anawashukuru wanaCCM wote wa Kibaha Vijijini kwa kuendelea kumuamini na kumpa kura nyingi zilizompa ushindi mkubwa huku akiahidi kuendelea kushirikiana vyema katika kukijenga chama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news