Mbunge Mtenga atoa mapendekezo kabambe miundombinu, elimu,kilimo na viwanda

Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini mkoani Mtwara, Hassan Mtenga amesema kuwa,tafakari ya kina inapaswa kufanyika kabla ya kuchukua maamuzi ya kujenga miundombinu hususani madaraja ya gharama kubwa ili kuweza kutoa huduma kwa Watanzania wengi na wageni kutoka nje ya nchi, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga akichangia hoja katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 9, 2021. (Picha na Mwandishi DIRAMAKINI).

Pia amezishauri Wizara ya Kilimo kwenda kuangalia namna ya kuwajengea uwezo wakulima mkoani Mtwara ambao wanazungukwa na vyanzo vya asili vya maji, lakini uzalishaji bado upo chini kutokana na ukweli kwamba hawana uelewa wa kitaalum juu ya kilimo biashara.

Ameyasema hayo leo Aprili 9, 2021 wakati wa kujadili Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano Bungeni jijini Dodoma ambapo pia ametoa mapendekezo ya kuboresha mpango wa elimu bure na namna ya kuvifanya viwanda hapa nchini kuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mtenga amechukua nafasi hiyo kumpongeza Waziri wa Fedha, Dkt.Mwingulu Nchemba kwa kuja na mpango ambao unaonyesha mwelekeo mzuri.

"Lakini nina mambo ambayo ninaweza nikachangia kwenye maeneo kama matatu tukianzia kwenye miundombinu, kama tunahitaji tuvuke kutoka umaskini kwenda uchumi mkubwa, tunaponzungumza miundombinu hasa kwenye maunganisho ya nchi yetu, Kusini mwa Tanzania, kule Mtwara huwa ninaishukuru Serikali kwa kutujengea daraja la Mtambaswala, lakini huwa ninatoa angalizo,daraja hili limetengenezwa kwa gharama kubwa sana, lakini kwenye utengenezaji wake na matumizi ni tofauti.

"Nataka nieleze uhalisia, kutoka Mtwara kuelekea Masasi kuna kilomita zaidi ya 230, kutoka Masasi hadi daraja la Mtambaswala kuna kilomita zaidi 130, Mtambasawala hadi Boda kuna kilomita zaidi ya 75, Boda hadi Behira Nampula kilomita zaidi ya 788, hoja ni vipi,pale Mtwara ukitoka Mtwara kuelekea Ruvuma kuna kilomita zaidi ya 70, Ruvuma hadi Nsimbwa-Nampula kuna kilomita zaidi ya 445, kama tungejenga daraja hili kupitia pale Mto Ruvuma, tungeweza kufungua mawasiliano kati Msumbiji na Tanzania, Afrika Kusini kupitia Msumbiji kuja Tanzania.

"Kwa sasa ndugu zetu wa Afrika Kusini wakitaka kwenda kuuza magari wanapitia Zambia ambapo wanatumia zaidi ya kilomita 2800 kuja Tanzania, hapa ninataka kusema kuwa hapa hauhitaji digrii wala maprofesa, ni suala la uamuzi sasa kwa waziri mwenye dhamana kulifanyia kazi suala hili,"amefafanua Mbunge Mtenga.

Pia amempongeza Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kuonyesha bidii kubwa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima nchini.

Mbali na pongezi hizo, ameshauri kuwa kule kwao Mtwara kuna eneo ambalo linaitwa Kitele, eneo ambalo amelishuhudia tangu akiwa mtoto hadi sasa anaelekea uzeeni ambalo limekuwa linamwaga maji ambalo ni chemchem ya kutosha na linaweza kutumika ipasavyo kwa ajili ya kilimo biashara.

Amesema, wananchi wamekuwa wakilima mpunga ambao hauna tija kubwa, hivyo anaiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kufika hapo ili kuona namna ya kuwasaidia wakulima waweze kuzalisha kwa faida zaidi.

"Twendeni mkajionee ili muweze kuleta kilimo biashara. Hakuna skimu za umwagiliaji, wakati ule mpunga ni mzuri sana,"amesema Mheshimiwa Mtenga.

Akizungumzia mpango wa elimu amesema kuwa,Serikali inapaswa kupata pongezi kwa kuwekeza vilivyo katika mfumo wa elimu bila malipo.

Hata hivyo, amesema licha ya mafanikio hayo bado kuna tatizo, kwani shule ya msingi kila kichwa cha mwanafunzi wanapeleka shilingi 6000 huku kwa upande wa sekondari kila kichwa wanapeleka shilingi 10000 kiasi ambacho ni kidogo kulingana na mgawanyiko wa mahitaji.

Amesema, fedha hizo tayari wizara wanazipelekea zikiwa na mgawanyo unaanzia asilimia 10 ya utawala, michezo asilimia 20, mitihani asilimia 20, vifaa asilimia 30 kwenye fedha hizo na ukarabati asilimia 20.

Amesema, kiasi hicho cha fedha ni kidogo sana, hivyo kusababisha walimu kutumia njia mbadala kuwafaulisha watoto ili mradi tu waonekane wanasoma.

Amesema, shule nyingi wazazi wamekuwa wakichangia, lakini wengi wao wamekuwa wakigoma kwa sababu myumbulisho wa hizo fedha hawauelewi.

Amesema kuwa, Wizara ya Elimu ina wajibu wa kuongeza ruzuku ya kutosha kwa ajili ya kufanikisha elimu bila malipo kwa ajili ya kuleta tija kubwa zaidi.

Akizungumzia, kuhusu suala la viwanda amesema kuwa, kule Kusini kuna kiwanda kikubwa cha Dangote ambacho kimetoa ajira zaidi ya 6,000, "Kimetoa ajira za kutosha, lakini kinashindwa kusonga mbele kutokana na kodi za TRA". "Hapa karibuni mlikuwa mnasikia kwamba kiwanda cha Dangote kinataka kufungwa, hii ni kutokana na gharama kwani wamechoka,"amesema.

Amesema, kwa mfuko mmoja wa saruji ambao unauzwa kwa shilingi 11,000 TRA wanachukua kodi ya shilingi 3000 hivyo kusababisha gharama za uendeshaji ndani ya kiwanda hicho kuwa kubwa zaidi.

Amesema, mkanda mmoja wa mashine unapoharibika unatumia zaidi ya shilingi milioni 180 kuagiza na kuufunga. "Hivyo inatupasa kuchukua hatua ili kuvisaidia viwanda vyetu ili kuboresha uchumi wetu,"amesema.

"Hivi karibuni mimi mwenyewe nimezungumza na wawekezaji kutoka nje zaidi ya sitra, lakini wanasema Mtenga ili suala kwenu haliwezekani, kwani ukitaka kufungua kiwanda Tanzania shughuli zake si ndogo.

"Ukitaka kufungua kiwanda kuwa mwekezaji, shughuli zake si ndogo, kuna watu zaidi ya nane hadi tisa, ukitaka kiwanda unamkuta NEMC, TBS, TRA, lakini kuna janga kubwa la Kitaifa linaitwa NIDA leo mwekezaji ametoka nje, kadi ya NIDA anaipata wapi hapa Tanzania, kuna mtu anaitwa OSHA, kuna mtu anaitwa Zimamoto vile vile kuna suala la kibali cha kuishi, ukitaka kwenda kurenew kibali cha kuishi japo miaka miwili utatumia zaidi ya miezi nane hadi tisa kukipata, yupo mtu mmoja hapa anaitwa Mkurugenzi wa NEMC, yaani afadhali leo uanaweza kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukampata, lakini si huyo Mkurugenzi.

"Naomba kushauri hizi taasisi zikae pamoja kuona ni namna gani ambavyo zinaweza kutoa huduma bora kwa pamoja kwa ajili ya kuwezesha mipango ya Serikali kutekelezeka kwa wakati na kwa mafanikio,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news