Mbunge Neema Lugangira, Rais wa DICOTA wakabidhi vipima oksijeni vitakavyosaidia mikoa 11

Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs),Mhe.Neema Lugangira na Rais wa Baraza la Watanzania wanaoishi Marekani (DICOTA),Dkt.Frank Minja wamekabidhi msaada wa Vipima Oxijeni (Pluse Oximeters) 108 kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa ajili ya Vituo vya Afya kutoka Mikoa 11 ikiwa ni mchango wao katika kuthamini juhudi za Serikali katika kuimarisha afya za Watanzania.
Rais wa DICOTA, Dkt.Frank Minja,Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Masuala ya Afya; Mhe Dkt Festo Dugange,Naibu Katibu Mkuu Afya na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs), Mhe. Neema Lugangira wakifungua vipimo vya Oxijeni ili kujaribu ufanyaji kazi wake.

Msaada huo umepokelewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Masuala ya Afya; Mhe Dkt Festo Dugange ambapo vifaa hivyo vitagawiwa katika mikoa ya Dar-es Salaam, Dodoma, Kigoma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Lindi na Njombe.  

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo wa vifaa, Mbunge wa NGOs Tanzania Bara, Mhe.Neema Lugangira alimshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe Ummy Mwalimu kwa ushirikiano mkubwa aliowapatia katika kufanikisha shughuli hiyo ya leo.

Mbunge Neema Lugangira alisema pia wanashukuru Dkt Grace Maghembe, Naibu Katibu Mkuu na Dkt Ntuli Kapologwe, Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Afya, Lishe kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wamekuwa wakiendelea kuwapatia.

“Sisi tunamshukuru sana Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu, kuridhia kupokelewa kwa msaada huu, ambao umepokelewa na Naibu Waziri, Dkt. Festo Dugange. Mimi kama Mbunge nitaendeleza jitihada hizi kwa niaba ya Serikali ili lengo la kuimarisha Afya ya Mtanzania iweze kutimia,”amesema Lugangira.
Awali akizungumza wakati akiipokea msaada huo wa vifaa tiba ambavyo vinatumika kupima kiasi cha Oxijeni katika mwili wa mwanadamu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya, Mhe Dkt. Festo Dugange amewapongeza Watanzania hao waishio Marekani kwa kuthamini juhudi za Serikali ya Nchi yao za kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya afya nchini. 

Alisema ili kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa kikamilifu, Naibu Waziri ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2021/22 serikali imetenga shilingi bilioni 65 kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba. 

“Serikali imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa Miundombinu na katika mwaka wa fedha 2021/22 tumeweka kwenye bajeti ya dawa na vifaa tiba kama hivi na vingine kiasi kinachofikia Bil.65, hivyo kwa jitihada hizi za wadau hawa na wengine wote watakao kuja hapo baadaye ni ishara kwamba lengo letu la kuweka vitendanishi na dawa litatimia,” amesema Mhe Naibu Waziri Dkt. Dugange.

Akiongea kwa niaba ya Watanzania waishio nchini Marekani, rais wa DICOTA, Dkt. Frank Minja, amesema, wanaona fahari ya kuchangia vifaa hivyo ambavyo vitakwenda kugawiwa kwenye ngazi ya Hospitali za Wilaya na kutumika na watanzania wenzao na kuahidi ni mwanzo ambapo wanatarajia kufanya mengi zaidi kwa kushirikiana na Serikali na Mbunge Lugangira katika Sekta hii ya Afya.  

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe, amesema kuwa atahakikisha kuwa vifaa vilivyopokelewa vinatunzwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu. 

Hafla ya kukabidhi vifaa tiba ilifanyika Makao Makuu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI jijini Dodoma na kuhudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe na Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu Paulina Mkwama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news