Jamhuri ya Rwanda imeanza wiki ya kumbukumbu ya maombolezo ya mauaji ya kimbari yaliyotokea katika nchi hiyo miaka 27 iliyopita.
Huu
ni mwaka wa pili sasa kumbukumbu za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi
wa Rwanda zikifanyika katika hali isiyo ya kawaida kutokana na kuwepo
kwa janga la corona.
Rais Paul Kagame wa Rwanda akiwasham mshumaa wa matumaini. (Picha na Reuters).
Zoezi
lilianza jana ambapo Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliwaasha mshumaa wa
matumaini ambapo utawaka kwa siku 100 sawa na muda ambao yalidumu mauaji
hayo.
Rais
Kagame alisema, hakuna wakati hata mmoja ambao nchi yake imeweza kuwa
pamoja zaidi ya wakati huu, lakini akasema mafanikio hayo bado
yanakumbwa na changamoto kutoka kwa baadhi ya nchi za nje.
"Baadhi
ya hawa watu pale walipo wakijaribu kuandaa masomo kwetu sisi, kuhusu
jinsi demokrasia inavyoendeshwa na haki za binadamu. Lakini wakati huo
huo unakuja wao hao hao wakiwakumbatia wale waliofanya mauaji haya
tunayo yakumbuka hii leo. Wanawalinda,wanawasemea na kuwasaidia huku
wakisema hawa ndiyo watu wanaotaka kuibadili Rwanda,"alisema Kagame.
Kumbukumbu
za mauaji hayo zimefanyika huku kukiwepo na itikadi za mauaji hayo
zinazoendelea kusikika huku na kule ulimwenguni kutoka kwa wale
wanaotajwa kama wapinzani wa Serikali ya Rwanda lakini ambao serikali
inashikilia walihusika kwenye mauaji hayo. Rais akiwazungumzia hao pia
na kwa kutumia lugha ya mafumbo amesema
"Yaani
ni jambo la kuvutia unapowaona mataifa hayohayo yakiwakamata watu hao
kwa makosa kwa mfano ya ubakaji au wizi wa pesa waliofanya katika nchi
hizo zilizowakumbatia na wanapofikishwa mahakamani bado utazisikia sauti
zinazosema, imesababishwa na maagenti wa Kagame, hivi ni kwa jinsi gani
unaweza kwenda kwenye nchi ya kigeni na kumlazimisha mtu kulifanya kosa
la ubakaji au kosa la wizi? Lakini unakuta haya yote tunakuwa
tumeyasema mapema bila kusikilizwa kwa sababu za kimaslahi,"alisema.
Rais
Paul Kagame alisema, ukweli kwamba bado kuna miili ya waathirika wa
mauaji inayoendelea kuokotwa hapa na pale miaka 27 iliyopita ni ishara
nyingine, huku akisema serikali yake na wananchi kwa ujumla hawatakubali
kufumba macho wakati waliofanya hayo wakiendelea kubeza kutokea kwa
mauaji hayo.
Awali
ilizoeleka watu kukusanyika katika maeneo mbalimbali, lakini safari hii
hilo halikuwepo kutokana na kupambana na maambukizi ya virusi vya
corona.
Rais Kagame alisema, kwamba hali hii imesababisha machungu zaidi kwa manusura lakini akawapa matumaini kwamba huenda ikaisha.
Rwanda
inaendelea kutoa chanjo ya corona kwa wananchi wote hali ambayo kwa
kiasi fulani imeleta matumaini miongoni mwa wananchi.Kumbukumbu
zilizoanza leo zitaendelea kutimia siku mia moja muda ambao mauaji hayo
yaliyoua zaidi ya watu milioni moja yalidumu.
Tags
Kimataifa