Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema kuwa Watanzania wana imani kubwa na chama hicho katika kuwaletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, anaripoti Amos Lufungilo (DIRAMAKINI) Mara.
Kada ya chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph. (Picha na Amos Lufungilo/ DIRAMAKINI).
Amesema, mpaka sasa katika Taifa la Tanzania hakuna chama kingine ambacho kinaweza kushindanishwa na CCM kutokana na uimara wake, uthabiti, pamoja na utekelezaji madhubuti wa ilani katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maendeleo katika maeneo yao na hivyo alisisitiza wananchi kuzidi kukiamini na kutembea kifua mbele kutokana na Chama Cha Mapinduzi kuwa imara.
Katika mahojiano na Mwandishi DIRAMAKINI Mjini Musoma pamoja na mambo mengine,Mwalimu Makuru amesema kuwa, falsafa ya CCM ilijengeka kutoka katika vyama vya ukombozi vya ASP na TANU ambayo ilikuwa imejikita katika utetezi wa wanyonge na mpaka sasa kimeendelea kupigania haki za wanyonge na kuzidi kukipa hadhi na mvuto mkubwa wa kupendeka kwa Watanzania wote.
Pia amesema, maendeleo yaliopo nchini kwa sasa ni matunda mazuri na uimara thabiti wa CCM katika kuwajali wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo mbalimbali yakiwemo ya kijamii ambayo ni utekelezaji wa ujenzi wa vituo na hospitali za wilaya na mikoa, utoaji elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari na hivyo kuwavutia wananchi wengi wanyonge kumudu kusomesha watoto wao, ujenzi wa miradi mikubwa ya maji mijini na vijijini hatua ambayo imewafanya Watanzania kuzidi kukipenda, kukiheshimu na kukithamini kila kukicha.
Mwalimu Makuru amesema upande wa kiuchumi Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kimelifanya Taifa liheshimike ndani na nje ya mipaka ikiwemo kuimarisha huduma ya umeme nchini kwa kujenga miradi mikubwa ya umeme na kupeleka huduma ya REA Vijijini, ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli, ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa masoko, upanuzi na ukarabati wa bandari mbalimbali nchini ili kuimarisha huduma za uchukuzi kwa maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kada huyo ameongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi ndicho chama pekee ambacho kinaaminika kwa Watanzania kutokana na kuyatekeleza mambo mengi yenye afya kwa wananchi na Taifa hivyo kinapaswa kuendelea kuwa imara na kutokuwa na migawanyiko ya aina yoyote ambayo inaweza kukiletea taswira hasi kwa wananchi ambao wanakiamini na kukitegemea kwa maendeleo yao hivyo, Wana CCM aliwaomba ndani ya chaguzi kusiwe na makundi pindi chaguzi ndani ya chama hicho zinapomalizika.
Mwalimu Makuru amesema kuwa, CCM ndicho chama chenye demokrasia komavu nchini kwani katika chaguzi zake za ndani watu hupata fursa ya kugombea nafasi ndani ya chama na jumuiya zake na kukiacha chama kikiwa salama na wana CCM huendelea kuwa wamoja Jambo ambalo limezidi kukiimarisha na kukifanya kiendelee kuwaongoza Watanzania.
"Mfumo madhubuti wa kiuongozi ndani ya CCM umeendelea kukifanya kiwe imara, mfano kiongozi au mwanachama yeyote yule akifanya Jambo kinyume na kanuni na taratibu za chama huwa hawasiti kumchukulia hatua kali za kinidhamu bila kujali hadhi yake na uwezo alionao kiuchumi. Jambo hili ni jema sana. Na ndiyo maana tumeshuhudia katika awamu zote viongozi wa chama waliokwenda kinyume waliwajibishwa na kuonywa huku wengine wakikemewa hadharani kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya chama na Taifa kwa ujumla,"amesema Mwalimu Makuru.
Mwalimu Makuru amewaomba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi wote kuendelea kumuamini Rais Samia Suluhu Hassan kuwa atazidi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa Taifa.
Pia wamwamini kuwaongoza vyema pindi atakapothibitishwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho katika kukiongoza kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi mapana ya chama na Taifa kwa ujumla kama awamu nyingine zilizopita za marais kuwa wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi ili kusukuma maendeleo kwa wananchi kwa kasi.
Mbali na hayo, Mwalimu Makuru amewasisitiza Watanzania kuendelea kudumisha tunu za Taifa ikiwemo amani na mshikamano, utengamano wa Kitaifa na kuwa wazalendo huku viongozi wa umma wenye dhamana ya kuwatumikia wananchi akiwahimiza kuwa waadilifu na wafanye kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi pasipo kujali dini,chama au kabila.
Tags
Habari