Mzee Mwinyi:Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye amempongeza kwa kuanza vizuri majukumu yake ya kuongoza nchi, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).

Akizungumza baada ya mazungumzo yao leo Aprili 12, 2021,Rais Mwinyi amesema amefika nyumbani kwa Rais Samia jijini Dar es Salaam kumjulia hali, kumtia moyo na kumhakikishia kuwa yeye na wazee wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano na kumsaidia wakati wowote watakapohitajika kufanya hivyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alifika kumsalimia Rais Samia Nyumbani kwake jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Aprili, 2021. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alifika kumsalimia Rais Samia Nyumbani kwake jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Aprili, 2021. Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan nyumbani kwake. (Picha na Ikulu).

“Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more...ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha, kila raia unayemsikia anasema Mama ameanza vizuri, tuliyekuwa nae tulikuwa na Rais mzuri sana, mzoefu wa mambo ya kiserikali, ametufanyia kazi nzuri sana.

"Sasa kaacha mambo haya ghafla kamuachia mwenzie, sasa Mama naye mwanadamu atakuwa na yake na vile vile kuna mambo ambayo yameanzwa na mtu mwingine ambayo watu wanayataka wanayapenda, wanamshikilia Mama tunayataka haya tunayataka, tulieni tutayatekeleza haya, sasa hilo linafurahisha,”amesema Rais mstaafu Mwinyi.

Rais mstaafu Mwinyi amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa kuacha balaa, ugomvi na fitina badala yake wawe na umoja, mshikamano na kufanya juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news