Rais Dkt.Mwinyi: Atakayethubutu kupandisha bei ya bidhaa, atawajibishwa

Serikali imeahidi kuchukua hatua kali kwa mfanyabiashara yoyote atakayebainika kupandisha bei za bidhaa au huduma kwa utashi ama tamaa bila ya kuwepo sababu ya msingi kwani tayari imeshatoa bei elekezi za bidhaa muhimu za chakula, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema hayo leo Aprili 12, 2021 katika risala yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan mwaka huu 2021 Miladia sawa na mwaka 1442 Hijria.

Katika risala yake hiyo, Alhaj Dkt.Mwinyi amesema kwamba, kwa pamoja ni vyema wananchi wenye kipato cha chini wakafikiriwa hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mahitaji ya familia yanaongezeka.

Amesisitiza kwamba, kwa msingi huo huo, wafanyabiashara wa bidhaa zote zikiwemo za nguo ni vyema wakazingatia uwezo wa wananchi kwani kuwakatia nguo watoto katika kipindi hiki kwa ajili ya Sikukuu ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wote wa Zanzibar.

Ameongeza kuwa, inafurahisha kuona kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto za usafirishaji na upatikanaji wa biadhaa mbalimbali, shughuli za biashara na upatikanaji wa chakula hapa nchini zinaenda vizuri ambapo bidhaa zote muhimu zinapatikana wakati huu mwezi wa Ramadhani ukikaribishwa.

Alhaj Dkt.Mwinyi amesema kuwa taarifa za Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo inatoa matumaini ya kuwepo kwa chakula cha kutosha yakiwemo mazao ya muhogo na ndizi ambayo hutumiwa na wananchi wengi kwa futari katika mwezi wa Ramadhani.

Aidha, Alhaj Dkt.Mwinyi amesema kuwa Machi 4, 2021 alikutana na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza chakula na kuwataka washirikiane na Serikali kufanya maandalizi mazuri katika kuhakikisha kwamba bidhaa zote hasa za chakula kwa wananchi wa Zanzibar ziweze kupatikana katika kipindi chote cha mwezi wa Ramadhani na baada ya hapo.

Alhaj Dkt.Mwinyi ameeleza kwamba, kwa hakika ibada ya Saumu ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchamungu, jambo ambalo ni jema na linaleta manufaa hapa Duniani na kesho Akhera.

“Kwa hivyo, tuukaribishe Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa furaha na matumaini na tujiandae kunufaika kutokana na neema na fadhila mbalimbali zilizo katika kipindi chote cha Mwezi huu tunaoukaribisha,”amesema Alhaj Dkt. Mwinyi.

Pamoja na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu kuhimizana kutekeleza ibada za Faradhi sambamba na kukithirisha ibada za Sunna ili kupata radhi za Mola ambapo miongoni mwa ibada iliyosisitizwa zaidi kufanywa kwa wingi katika mwezi wa Ramadhani ni kusoma Qur-an tukufu.

Ameeleza kwamba katika kutafuta fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani imehimizwa kujitahidi sana kutekeleza ibada ya sala zote za Faradhi na sala za Sunna, kuomba dua, kusoma nyiradi mbali mbali, kufanya itikafu, na kutekeleza Sunna nyengine zinazoambatana na Mwezi wa Ramadhani.

Ameongeza kwamba, jambo jingine linalohimizwa kutekeleza zaidi ndani ya Mwezi wa Ramadhani ni kutoa sadaka hasa kwa watu wenye mahitaji,yatima,wazee,masikini na mafakiri ibada ambayo inaongeza baraka na mahusiano mema katika jamii.

Alhaj Dkt.Mwinyi pia ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi pamoja na viongozi na watumishi wa manispaa zote nchini juu ya umuhimu wa kuzingatia usafi katika miji hasa katika masoko na maeneo yanayohusika na uuzaji wa vyakula ilikujiepusha na maradhi ya mlipuko.

Kadhalika, amewahimiza viongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha huduma za maji zinawafikia wananchi hasa katika maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani kwa uhakika.

Amewataka Masheha wa Shehia ambazo zina matatizo ya maji wawasiliane na (ZAWA) ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa zikiwemo kuwapelekea wananchi magari ya maji kwa lengo la kuondokana na usumbufu wa kupata huduma hiyo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt.Mwinyi amewahimiza viongozi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo sheria za usalama barabarani wakati wote na kuongeza nguvu hasa katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya usafiri huongezeka.

Amewataka kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva watakaojaribu kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kwenda mwendo kasi pamoja na wale wenye tabia ya kuwasumbua wananchi kwa kuwashusha bila ya kuwafikisha mwisho wa vituo vilivyopangwa na Serikali.

Hata hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi amewakumbusha wananchi wenye dharura maalum na wale wasiokuwa Waislamu waendeleze utamaduni wa kujizuia kula hadharani, kutovaa nguo zisizoendana na maadili ya Kizanzibari sambamba na kuepuka matendo yatakayowakwaza Waislamu wenye kutekeleza ibada ya funga.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisoma risala kwa wananchi kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka 2021,sawa na Mwaka 1442 Hijria, kupitia vyombo vya habari katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news