Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulihutubia Taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya Alhamisi ya April 22,2021.
Kwa muyjibu wa taaifa za awali, Rais Samia atafanya tukio hilo la kulihutubia Taifa kupitia Bunge jijini Dodoma kuanzia saa 10 jioni.
Aidha, kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa Kikatiba Rais ni sehemu ya Bunge hivyo anaweza kulihutubia Bunge wakati wowote.
Kwa nyakati tofauti wachambuzi wa mambo wamemweleza MWANDISHI DIRAMAKINI kuwa, hotuba ya Rais Samia inasubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania ikizingatiwa kwamba, hii itakuwa ndiyo hotuba yake ya kwanza kwa Taifa tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Machi 19, 2021.
Ni baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kufariki dunia Machi 17, mwaka huu wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo mkoani Dar es Salaam.
Hayati Dkt.Magufuli alizikwa nyumbani kwake mwezi Machi 26, mwaka huu huko wilayani Chato Mkoa wa Geita.
Miongoni mwa wachambuzi hao amesema kuwa, "matamanio ya wengi ni kupata dira na mwelekeo rasmi wa Taifa letu, kwani hata huko bungeni licha ya kipindi hiki muhimu kwa ajili ya kujadili bajeti kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa letu, wengi wao waheshimiwa wabunge wameamua kujikita zaidi kujadili masuala ambayo si kwamba hayana umuhimu sana, ila kwa wakati huu wanapojadili wanaonekana kwa Watanzania kuwa wamepoteza mwelekeo, hivyo hotuba ya Rais itatupa dira kamili,"amesema Mchambuzi huyo.
Hata hivyo, taarifa ya Rais kulihutubia Bunge imethibitishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai huku akiwataka wabunge wote kuwepo bungeni.
Tags
Habari