Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi.Kimbunga Jobo kimeendelea kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo usiku wa kuamkia tarehe 24/4/2021 (Jumamosi) kimbunga hiki kinatarajiwa kuwa umbali wa takriban kilomita 235 mashariki mwa kisiwa cha Mafia.
Jumamosi mchana kimbunga Jobo kinatarajiwa kuwa umbali wa takribani kilomita 125 mashariki mwa Mafia.
Aidha, usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 25 Aprili 2021, kimbunga Jobo kinatarajiwa kuendelea kupungua nguvu na kuwa mgandamizo mdogo wa hewa kikiwa katika mwambao wa pwani ya Tanzania.
Vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 hadi 60 kwa saa, mawimbi makubwa baharini pamoja na ongezeko la mvua kwa maeneo ya ukanda wa pwani vinatarajiwa kujitokeza.
Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja kutokana na kimbunga Jobo ni pamoja na mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja. Aidha, maeneo mengine yanayotarajiwa kuathirika ni mikoa ya Mtwara, Tanga pamoja na kisiwa cha Pemba.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko/ vipindi vya mvua kwa maeneo mengine yaliyo mbali na ukanda wa pwani (ikiwemo ukanda wa Ziwa Victoria).
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Tags
Habari