Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ametoa wito kwa Mahakimu na Wasajili kote nchini kuacha kupokea ama kusajili Mahakamani mashauri yasiyo kuwa na tija ili kupunguza kulundika kesi zisizo na msingi kwa lengo la kuwapunguzia wananchi usumbufu usio wa lazima na kwa kufanya hivyo Mahakama itaendelea kuchochea uchumi na kuleta amani kwa watu wake,anaripoti Innocent Kansha, (Mahakama Njombe).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe, Wengine Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mwandisi Lubilya Marwa (wa tatu kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente (wa kwanza kulia) Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (wa pili kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Said Ding'ohi.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Njombe lililozinduliwa rasmi na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi Aprili 27, 2021
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifunua kibao kuashiria uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe, Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mwandisi Lubilya Marwa (wa katikati aliyeshika kitambaa) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente akishuhudia (wa kwanza kushoto).
Akizindua rasmi Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ya Njombe mnamo Aprili 27, 2021 Mhe. Dkt. Feleshi alisema Hakimu au Msajili unapoletewa hati ya shauri jipya liwe la Madai au Jinai unatakiwa upokee shauri lenye sifa ya kusikilizwa na kama shauri halikidhi vigezo unatakiwa kutumia amri za awali “Initial Orders” kwa mujibu wa sheria kulimaliza shauri hilo lililopo mbele yako ama kwa kulirudisha likafanyiwe marekebisho au likafanyiwe upelelezi wa kina.
“Kabla hujatoa amri ya kuita watu Mahakamani jiulize kama hati hiyo ya madai umeisoma na umeielewa na kwa upande wa jinai Hakimu tumia sheria ya mwenendo wa makossa ya jinai kuona kama shauri linakidhi vigezo vya kupokelewa na kusajiliwa Mahakamani, hii itasaidia kupunguza mashauri kukaa Mahakamani muda mrefu pasipo kuwa na ulazima bila kusikilizwa”, alisistiza Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi alisema ni rai yake kwa Mahakimu kuwa yale mashauri ya jinai yasiyokuwa ya makosa makubwa yanapopokelewa Mahakamani siku hiyo hiyo mshitakiwa asomewe mashitaka na hoja za awali ili kesi ianze kusikilizwa wakati huo huo.
Aidha, Jaji Kiongozi aliongeza kuwa Mahakama kwa sasa itaanza kushughulika na Mahakimu wanaopokea kesi sizio na hadhi ya kupokelewa Mahakamani kwani eneo hili ni moja ya maeneo ya kiukaguzi na kwa kutambua kuwa Mahakama inao wajibu wa kutoa elimu kwa watu wanaoleta kesi za namna hii kwa kutoa ufafanuzi wa kwa nini mashuri ya namna hiyo yasipokelewe Mahakamani kupitia Maafisa Masjala.
Jaji Kiongozi alitumia wasaa huo kutoa ushauri kwa wadau wa Mahakama kuwa kila eneo lenye mamlaka ya kiutawala na idadi kubwa ya watu kwa maana ya makazi mengi kuwe na gereza dogo la Mahabusu ili kuisaidia Mahakama kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi kwani Mahakama kama taasisi tayari inayo miundombinu ya kutosha ya kusaidia kutoa huduma.
Ikumbukwe kwamba kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe mwaka 2012, kupitia Tangazo la Serikali Na. 9 la tarehe 01/03/2012 wananchi wa hapa Njombe na wilaya zake, ambazo ni Njombe, Ludewa, Makete na Wanging’ombe, walilazimika kusafiri umbali wa kilomita 223 kufuata huduma za Mahakama ngazi ya Mkoa, mkoani Iringa, aliongeza Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi, aliongeza kuwa umbali huo ulikua mrefu na wananchi waliathirika kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta huduma za Mahakama, muda ambao wangeutumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Lakini pia, umbali huo kwa namna moja au nyingine uliwakatisha tamaa baadhi ya wananchi kufuatilia haki zao Mkoani Iringa na wengine hawakuweza kumudu gharama za kujikimu, hivyo kukosa haki zao.
Wananchi walio wengi katika Mkoa huu ni Wakulima, wafanyabiashara na Wafugaji, jamii ambayo kwa hakika inahitaji muda mwingi ili waweze kujikita katika shughuli zao za kiuchumi. Uwepo wa jengo hili jipya ni nafuu na ukombozi kwa wananchi wote wa Njombe kwani litaokoa muda na fedha ambazo wanachi walikuwa wakipoteza hapo awali, aliongeza Dkt. Feleshi.
Akiendelea kufafanua Jaji Kiongozi alisema moja ya mikakati iliyowekwa na Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa kila eneo jipya la kiutawala linaloanzishwa, kunajengwa Mahakama, kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za umma. Serikali inapoanzisha Mkoa, Wilaya, Tarafa na hata Kata mpya ni kwa sababu kwamba wananchi wa maeneo hayo wanahitaji huduma za Serikali kwa ukaribu na wepesi zaidi. Vigezo hivyo vinaonesha pia umuhimu wa kusogezewa kwa huduma za Mahakama karibu na wanachi.
Kwa sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe wanasajili wastani wa mashauri 524 kwa mwaka, pia Mkoa huu una mashauri mengi ya mauaji ambayo husikilizwa na Mahakama Kuu. Jengo hili linayo nafasi ya kutosha kuwezesha Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu kuendesha vikao vya Mahakama Kuu bila tatizo lolote.
“natoa rai kwa watumishi wa Mahakama kwamba, majengo haya ya kisasa na miundombinu bora, iambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa mwananchi. Niwasihi watumishi wenzangu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama nyingine hapa nchini kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma”, alisisitiza Dkt. Feleshi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiteta jambo na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa Njombe Mwandisi Lubilya Marwa (wa pili kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi, wengini ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente (wa pili kushoto), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Martin Chuma na (wa kwanza kulia) ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Mhe. Catharina Revocati.
Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na makunduzi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe.
Baadhi ya Wananchi waliohudhuria uzinduzi uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe wakisikiliza Hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani). Picha zote na Innocent Kansha - Mahakama.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Eng. Lubilya Marwa akitoa salamu za mkoa aliushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kukamilisha ujenzi wa miradi mitatu (3) ya majengo ya kisasa ya Mahakama katika Wilaya tatu kati ya nne za Mkoa wa Njombe.
“Uzinduzi wa Mahakama hizi tatu za Njombe, Makete na Wanging’ombe kwetu sisi ni tukio la kihistoria kwa kipindi kirefu Mkoa umekuwa ukifanya kazi zake kwenye mazingira magumu si kwa Mahakama tu hata Taasisi zingine na sasa Muhimili wa Mahakama utafanya kazi katika mazingira bora na rafiki”, alisema Mkuu wa Mkoa Eng. Marwa.
Eng. Marwa aliongeza kuwa ni imani ya Uongozi wa Mkoa kuwa hata Wilaya ya Ludewa iliyosalia na yenye changamoto kubwa itafikiliwa na kutengewa bajeti ili nayo iweze kupata Jengo lake la Mahakama hali itakayo imarisha utendaji wa shughuliza zake za kimahakama.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente alisema Mahakama ya Tanzania imepitia nyakati ngumu na historia ndefu kuhusu suala la majengo nyakati fulani Mahakama ilikuwa ikitoa huduma zake kwa kutumia majengo ya Chama Cha Mapindunzi hadi ilipofika mwaka wa 1992 kulipoanzishwa Vyama Vingi vya Siasa, Mahakama ikanza kusaka hifadhi huku na huku.
“Sisi kama Mahakama leo tunayofuraha sana kupokea jengo hili la kisasa nadhani hata wewe Mkuu wa Mkoa furaha uliyonayo haiwezi kulinganishwa na sisi wanamahakama kwa sababu kuna msemo unasema ‘Huwezi kulia msibani ukamzidi mama wa marehemu”, alisisitiza kwa bashasha Jaji Mfawidhi.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma aliwaomba watumishi wa Mahakama na wadau wote watakao tumia jengo hilo la kisasa kufanya kazi kwa bidii na huduma wakazotoa zisawiri muonekeno wa jengo husika, ikiwa ni pamoja na kutenda kazi kwa kuzingatia viapo vyao.
Tags
Habari