Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa serikali inakaribia kukamilisha mpango wa kuanzisha Mfuko Maalum wa Zakka ambao utatumika kuwasaidia watu wenye mahitaji visiwani Zanzibar.
Mheshimiwa Othman aliyasema hayo Aprili 23,2021 wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Masjid Swahaba ulioko Mtoni, kando kidogo ya Mjini Unguja, ambapo ameelezea jinsi ambavyo wale waliojaaliwa kuwa na kipato walivyo na wajibu wa kutoa sehemu ya kipato hicho kwa ajili ya wengine.
"Mwenyezi Mungu anawasifia wale wanaotowa miongoni mwa waja wake aliowaruzuku, lakini anaeleza kwamba hicho alichowaruzuku hakimaanishi kuwa ni chao. Bali wamepewa ili waweze kutowa. Na hakuna anayefilisika kwa sababu ya kutowa kwa wengine wenye uhitaji," alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais.
Mheshimiwa Othman amesema kuwa uamuzi wa kuwa na Mfuko wa Zakka ulishapitishwa tangu mwaka 2007 na kwamba utekelezwaji wake utawezekana hivi karibuni. Zanzibar ni nchi ambayo zaidi ya asilimia 90 ya raia wake ni waumini wa dini ya Kiislamu, jambo ambalo linaipa kila haki na wajibu wa kuwa na taasisi kama hiyo, ambayo itawasaidia waumini kutimiza moja ya nguzo muhimu sana za dini yao.
Pamoja na Waislamu wa ndani ya nchi, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema kuna matajiri wengine wa Kiislamu nje ya Zanzibar ambao wanataka sana kutowa Zakka zao kwa ndugu zao waliopo Zanzibar, lakini wamekosa chombo cha kuzikabidhisha Zakka hizo.
"Kwa kuwa na mfuko huu, hawa ndugu zetu walioko nje ya Zanzibar nao watakuwa na mahala wanapopaamini kuleta sadaka na zakka zao wakijuwa kuwa zitatumika kwa malengo waliyoyakusudia," aliongeza Mheshimiwa Othman.
Katika hatua nyengine, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kujitokeza bila woga kuwachangia ndugu zao wanaoendelea kushikiliwa katika magereza ya Tanzania Bara ambako wanakabiliwa na mashitaka ya ugaidi, maarufu kama Masheikh wa Uamsho.
Mheshimiwa Othman amesema si kosa kisheria kwa mtu yeyote kuwachangia washukiwa hao, kwani mbali ya wenyewe kuwa mikononi mwa vyombo vya dola, bado wana haki zao na wanahitaji kuwalipia mawakili wanaowatetea pamoja na kuziendesha familia zao.
"Tuendelee kuwasaidia ndugu zetu hawa kwa kila kile mtu atakachojaaliwa. Na sio kwa matunzo tu ya familia zao, lakini pia wana watu wanaowawakilisha mahakamani (mawakili). Kwa hivyo, ni wajibu kuwasaidia ili kuwapa nguvu wale wanaowasaidia mahakamani,"alisema.
Tags
Habari