Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2021 kwa kuwashindanisha wafanyakazi bora watatu (3) kutoka Idara za Ofisi hiyo ambao wamepatikana kwa kigezo cha utendaji kazi mzuri kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio ya Utendaji Kazi (OPRAS), anaripoti Mary Makapenda (Dodoma).
Mfanyakazi bora aliyechaguliwa ni Bw. Steven Mgala kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.
Akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amefafanua kuwa, wafanyakazi bora watatu (3) walioshindanishwa walipatikana baada ya mchujo wa Wafanyakazi bora 15 kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo utendaji kazi mzuri.
Mara baada ya wafanyakazi hao watatu kushindanishwa, Bw. Steven Mgala alipata ushindi akifuatiwa na Bw. Ally Ngowo kutoka Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ambapo hao wawili walishindanishwa tena, na Bw. Mgala kupata ushindi kwa mara nyingine.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Bw. Musa Joseph akimkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuzungumza na Watumishi wa Ofisi yake kabla ya kufanya uchaguzi wa mfanyakazi bora.
Akimtangaza mshindi huyo, Dkt. Ndumbaro alimpongeza na kuwashukuru watumishi kwa kufanya uchaguzi uliozingatia vigezo.
Kabla ya kufanya uchaguzi, Dkt. Ndumbaro, aliwataka watumishi kumchagua mtumishi ambaye utendaji kazi wake unaonekana kuwa ni bora badala ya kuchagua kwasababu za kufahamiana.
Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Utumishi, Bi. Flora Nyela, akitoa neno la shukrani na pongezi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alivyoendesha vizuri na kwa namna ya pekee zoezi la kumpata mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Steven Mgala akitoa neno la shukrani kwa Watumishi baada ya kuchaguliwa kuwa Mfanyakazi bora wa Ofisi.
“Tunapopiga kura, tusimchague mtumishi kwasababu unamfahamu au anatoka kwenye idara au kitengo kimoja, bali tumchague kwa utendaji kazi wake mzuri,” Dkt. Ndumbaro ameongeza.
Kwa upande wake, mfanyakazi bora aliyechaguliwa, Bw. Steven Mgala amewashukuru watumishi kwa kumuamini na kuona utendaji wake na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano kama kauli mbiu ya KAZI IENDELEE inavyohimizwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Tags
Habari