Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waajiri katika Taasisi za Umma kuhahakisha wanakuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi, yanayotekeleza wajibu wake kikamilifu ili kutoa haki ya ushirikishwaji kwa watumishi katika masuala muhimu yanayohusu ustawi wao, anaripoti Veronica Mwafisi (Dodoma).
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa umma jijini Dodoma.
Mhe. Mchengerwa amesema, amelazimika kuwaelekeza waajiri kuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi kwasababu amekuwa akipokea taarifa nyingi katika kipindi hiki kuwa yapo mabaraza yasiyofanya kazi wakati mabaraza yapo kwa mujibu wa sheria.
Ili kuhakikisha waajiri wanakuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuhakikisha katika mkutano wa baraza lijalo anampatia taarifa ya taasisi zote ambazo hazina mabaraza ya wafanyakazi kwani kutokuwa na mabaraza ni kuwanyima watumishi haki ya msingi ya kushirikishwa katika mambo muhimu yanayohusu mustakabali wa maendeleo yao ya kiutumishi.
Sanjari na hilo, amemtaka Mwenyekiti wa Baraza kumpatia taarifa ya Mabaraza ya Wafanyakazi ambayo hayafanyi kazi na vikao kwa mujibu wa sheria kwani kuwa na mabaraza ni jambo moja na kufanya vikao ni jambo jingine, hivyo mabaraza lazima yafanyike ili kutekeleza wajibu wake.
Mhe. Mchengerwa amesititiza kuwa, ofisi yake itafuatilia kwa karibu na itachukua hatua stahiki iwapo itabaini kuna uzembe umefanywa na waajiri ili kukwamisha uwepo wa Mabaraza ya Wafanyakazi au utekelezaji wa majukumu ya Mabaraza hayo.
Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma limeundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 30 (1) (2) cha Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma SURA 105.