WAZIRI GWAJIMA:SALAAM ZA SHUKRANI KWA WATEJA KWA KUTOA PONGEZI, MAONI NA KERO ZA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Ndugu Wananchi, Awali ya yote nachukua fursa hii kuwatakia watumiaji wote wa huduma za afya nchini Tanzania Heri ya Siku ya kumbukizi ya Hayati Abeid Amani Karume leo tarehe 7/04/2021. Tumkumbuke kwa ushujaa na uzalendo wake daima.
Aidha, napenda kutoa Shukrani kwa Wananchi wote ambao wamekuwa wakiwasilisha Pongezi, Maoni na Kero zao kupitia mifumo mbalimbali ya mawasiliano ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiwemo kwa barua, mitandao yetu ya kijamii, simu na ujumbe mfupi kupitia namba 199. Nikiri kuwa taarifa hizo zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kutambua maeneo yanayofanya vizuri na yale yenye changamoto.

Ndugu Wananchi, Vilevile, nawashukuru maelfu ya Wananchi ambao pale wanapoona hawakupata msaada kwenye ngazi ya Kituo, Halmashauri, Mkoa au Wizara kupitia namba husika zilizotangazwa wamekuwa wakizingatia kunitumia ujumbe mfupi kwenye simu yangu mimi Waziri ya 0734124191 kama nilivyoitangaza Disemba 19, 2020. 

Ndugu Wananchi, Napenda kuwakumbusha kuwa, kwa pongezi na kero za huduma za afya kamwe msikose mahali pa kusemea bali muendelee kutumia mifumo ya mawasiliano ya haraka huku mkizingatia maelekezo yaliyotolewa. Mahsusi kwa simu yangu Waziri wa Afya ya 0734124191 mawasiliano haya ni kwa ujumbe mfupi tu.

Nawahakikishia kuendelea kujibu na nikiona inafaa nitapiga simu au kutoa maelekezo kwa wasaidizi wangu wafuatilie na kusimamia jambo hilo na kunipa mrejesho.

Kwenu watumishi wataalamu wa afya, Natoa pongezi kwa wale wote ambao wamekuwa wakijituma kwa bidii kuwahudumia wateja wanaohitaji huduma za afya. Hakika kupitia maoni ya wateja tumeendelea kuwatambua watumishi wengi wenye moyo wa uzalendo na upendo katika kutimiza wajibu wao. Wale wenye changamoto nao tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni.

Ndugu Wananchi, Natoa Shukrani za dhati kwa ushirikiano wenu na tuendelee kushirikiana daima.


Dkt. Dorothy Gwajima.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,

JINSIA, WAZEE NA WATOTO.

07/04/2021.

Simu. 0734124191 (tuma ujumbe mfupi tu)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news